Magenge yawashambulia waafrika New Delhi
29 Machi 2017Mashambulizi hayo inasemekana yaanza kutokea baada ya kuenea uvumi kuwa mtoto mmoja wa kihindi ametekwa nyara na wanigeria wanaoishi katika mji huo.
Vurugu zilianza Ijumaa iliopita baada ya kijana mmoja wa kiume kupotea, nje ya New Delhi, na jamaa wa kijana huyo kusema kuwa ameuliwa na wanigeria. Magenge mjini humo yalianza kuwatafuta wanigeria wanaokaa katika sehemu hiyo na kuwashambulia baada ya baadhi wa watu kusema kuwa kijana huyo ameuliwa na watu waliomteka nyara.
Jumamosi asubuhi kijana huyo alirudi kwao, lakini alifariki baadae siku hiyo, ingawa mpaka sasa sababu ya kifo chake haijajulikana. Polisi wamewakamata wanigeria watano na wamewashutumu juu ya kifo na utekaji nyara wa kijana huyo. Lakini, baada ya masaa kadhaa, watu hao waliwaachiwa huru, huku polisi ikisema kuwa haina ushahidi wa kutosha.
Hatua zinazochukuliwa na Chama Cha Wanafunzi wa kiafrika New Delhi
Makundi ya wahindi yanaendelea kuwashambulia waafrika, mashambulizi ya hivi karibuni yalifanyika leo ambayo watu wawili wamevunjwa mifupa. Chama cha wanafunzi wa kiafrika kimewataka wanafunzi wote katika mji mkuu huo, wawe na hadhari na watoe onyo kali kwa wale wanaokaa katika mji wa Greater Noida wasitoke nje kwa sasa.
"Wanafunzi wote wanaosoma Greater Noida wametakiwa kukaa majumbani, wakati bado hali inaendelea kuzidi kuwa ya hatari.
''Tunawataka wawakilishi wote wa wanafunzi kutoka Afrika kuwaomba wanafunzi wote wabaki majumbani kwao," alisema mshauri wao. Wanafunzi wengi wamezima simu zao au wameacha kupokea simu kwa hofu walionayo juu ya hali hii na kuwepo kwa mashambulizi zaidi kwa siku zinazokuja.
Malaki ya wanafunzi wa kiafrica wanaishi na kusoma India, baada ya kuvutiwa na elimu bora na kuwepo kwa fursa zaidi za kazi nchini humo. Lakini upambanaji wa ubaguzi wa rangi, ni vita vya kila siku nchini humo ambako watu wenye ngozi nyeusi waonekana kuwa watu wachini kabisa.
Kawaida hali hii ya ubaguzi wa rangi nchini India imekuwa ikipuzwa na polisi na vyombo vya habari pia. Lakini hali hii ilibadilika mwezi wa tano mwaka jana, baada ya mwanafunzi kutoka Congo kushambuliwa alipotaka kupanda chombo cha usafiri kinachojulikana kama kibajaji au bodaboda New Delhi.
Wanaume watatu waliokuwa wakisisitiza kuwa wameuwahi usafiri huo, kwanza, walimpiga mwanafunzi huyo jiwe la kichwa na kumuuwa, polisi walisema. Mauaji hayo, yalisababisha wanafunzi wa kiafrika, wafanyabiashara na watu wa balozi mbalimbali kuandamana kutaka haki na usawa haraka iwezekanavyo. Mabalozi wa nchi za kiafrika mjini New Delhi walitoa tamko linaloitaka serikali ya India wazungumzie juu ya ubaguzi wa rangi nchi humo.
Usambaaji wa habari mbaya juu ya mashambulio ya hivi karibuni imemfanya waziri wa mambo ya nje wa India kuwatuma askari wawalinde waafrika wanaokaa katika mji mkuu huo .
Jumatatu waziri huyo wa mambo ya nchi za nje aliandika katika mtando wa kijamii wa twitter kuwa aliiomba serikali ya sehemu ya Uttar Pradesh ambako Greater Noida ndio ilipo wafanye uchunguzi juu ya machambulizi hayo haraka iwezekanavyo.
Mwandishi: Najma Said /ap
Mhariri: Gakuba, Daniel