Magenge yajaribu kuchukua udhibiti uwanja wa ndege Haiti
5 Machi 2024Hilo ni shambulio la hivi karibuni kabisa kwenye mfululizo wa hujuma za magenge ya wahalifu yanayolitikisa taifa hilo la kanda ya Karibia.
Duru zinasema watu wenye silaha walipambana kwa bunduki na vikosi vya usalama, katika uwanja wa ndege wa Toussaint Louverture uliopo kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.
Wakati makabiliano hayo yanatokea hapakuwa na ndege zozote uwanjani wala abiria.
Waandishi wa shirika la habari la Associated Press walishuhudia gari la kijeshi likiwa kwenye njia ya kuruka ndege likifyetua risasi dhidi ya makundi ya watu wenye silaha kuwazuia wasiingie katika viunga vya uwanja huo.
Inaelezwa kuwa shambulio hilo ndiyo kubwa zaidi kuwa kuulenga uwanja wa ndege katika historia ya Haiti.
Limetokea muda mfupi baada ya serikali ya Haiti kutangaza marufuku ya kutoka nje usiku na hali ya tahadhari ya muda wa saa 72 kufuatia kuongezeka kwa hujuma za magenge ya wahuni.