Magazetini
6 Machi 2018Kuna mambo mawili yaliyowashughulisha wahariri wengi wa magazeti ya Ujerumani. Kwanza ni uchaguzi wa bunge nchini Italia na mpango wa jeshi la Ujerumani Bundeswehr wa kutanua harakati zake dhidi ya kundi linalojiita dola la kiislamu nchini Iraq. Na kwanza gazeti la «Westfälische Nachrichten»kutoka (Münster) kuhusu uchaguzi wa Italia mhariri anasema.
Wataliana wamefanya maamuzi-Na kuchagua kile ambacho barani Ulaya kinaonekana kuwa matokeo mabaya kabisa.Kilichotokea Italia ni tarumbeta lililopulizwa na wanaounga mkono siasa kali.Kwa hakika ni ishara ya wazi kwa Ulaya.Na zaidi ya hilo ni mwiba na machungu makubwa kwa Berlusconi ambaye peke yake alijitapa na kujinasibu katika kampeini kwamba atawabwaga wenye siasa kali.Berlusconi ameshindwa na mara hii pengine ndio mwisho wake kabisa.
«Sächsische Zeitung» kutoka (Dresden) linasema
Haijalishi serikali ijayo mjini Rome itakuwa ya aina gani kilichodhahiri hapa ni kwamba Italia bado itabakia kuwa mshirika mgumu sana kwa Umoja wa Ulaya. Wakosoaji wakubwa wa siasa za Umoja wa Ulaya bado wana usemi mkubwa wa kisiasa nchini humo. Hapana shaka yoyote kwamba wataitumia nafasi hiyo kutia kishindo cha kudai mageuzi katika umoja huo. Matokeo ya uchaguzi wa Italia ni onyo kwa waliopo mjini Brussels. Kilichopo ni kwamba sio tu kuzisaidia nchi kifedha katika kuyatatua matatizo yao kijamii lakini pia kuziangalia changamoto zinazosababishwa na tatizo la uhamiaji.Katika yote hayo mawili Italia bado inajihisi kwamba Umoja wa Ulaya umeitupa mkono na kuiacha peke yake.Na kilichotokea nchini humo ni kama hatua ya kulipiza kisasi.
Ama kuhusu mpango wa kutanua harakati za kikosi cha Ujerumani nchini Iraq mhariri wa gazeti la «Stuttgarter Nachrichten» anawasiwasi.Anasema.
Kinachotaka kupendekezwa na bunge kesho Jumatano kuhusu kutanuliwa harakati za jeshi la Ujerumani Bundeswehr nchini Iraq kinaongeza kitisho katika sera ya usalama ya Ujerumani. Kwa kulifuata bunge hapana shaka jeshi la Ujerumani litalazimika kuzisimamisha harakati zake za kutowa mafunzo katika jimbo lenye mamlaka yake ya ndani la Wakurdi Kaskazini mwa Iraq. Na badala yake kikosi hicho kitabidi kiendeshe shughuli zake hizo kwa wanajeshi wa serikali kuu ya Iraq walioko kwenye eneo linalodhibitiwa na vikosi vinavyopambana na kundi linalofungamanishwa na dola la kiislamu:hiyo itamaanisha kwahivyo ni kufungua ukurasa mpya. Kwa maneno mengine Ujerumani inabadili sera zake nchini Iraq na kuzikaribia zile zinazofuatwa na Marekani na washirika wake NATO. Hata hivyo Ujerumani inabidi itambue kwamba gharama ya hatua hiyo ni kujiingiza zaidi katika mgogoro wa kikanda.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman