Magazetini: Waranti kukamatwa mkuu wa zamani wa Volkswagen
7 Mei 2018Mhariri wa gazeti la Nordwest-Zeitung la mjini Oldenburg , akiandika kuhusiana na waranti uliotolewa ili kukamatwa kwa mwenyekiti wa zamani wa kampuni ya Wolkswagen Martin Winterkorn anaandika kwamba msukumo wa hivi sasa dhidi ya mkuu huyo wa zamani wa Volkswagen unawaweka wachunguzi wa Ujerumani katika mbinyo mkubwa kuwa wazi. Mhariri anaendelea.
"Wamarekani wanatakiwa pengine kuangalia upya msingi wa mashitaka yao. Walifikia karibu sana na kumshitaki, kwa kuwa Winterkorn aliongoza kampuni hiyo na kuangalia kila shughuli iliyokuwa ikifanyika, katika utendaji wa hivi sasa na pia hapo kabla na kwamba alifahamu udanganyifu uliokuwa ukifanyika na pia hakuzuwia ama kupinga hatua hizo."
Kama hali hiyo ni sahihi, mkuu huyo wa kampuni hiyo ameshiriki katika hatua za kutengeneza vifaa ambavyo si sahihi, basi anakabiliwa na muanguko mkubwa.
Kuhusu mada hiyo hiyo mhariri wa gazeti la Badische Neueste Nachrichten anaandika kwamba mzozo mkuu hata hivyo si kati ya Martin Winterkorn, Volkswagen na mahakama: Mhariri anaandika:
"Hapana, mzozo huu ni baina ya mamilioni ya watu wanaomiliki magari yanayotumia mafuta ya dizeli kutoka katika kampuni hiyo ya Volkswagen, ambao wanakabiliwa na kitisho cha kuzuiwa kuendesha magari hayo. Volkswagen kama kampuni kwa hali hii inamakosa."
Gakuba:
Mhariri wa gazeti la Stuttgarter Zeitung anazungumzia kuhusu maandamano nchini Urusi dhidi ya rais Vladimir Putin. Mhariri anandika:
"Miaka sita iliyopita mamia kadhaa ya waandamanaji nchini Urusi walimiminika katika mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo. Lakini maandamano hayo sasa ni tofauti. Ni tofauti na yanapungua kasi , kwasababu wenye madaraka nchini Urusi hivi sasa wanaona kutumia nguvu ndio jambo muhimu ili kuzuwia watu kudai yale wanayoyaona kuwa ni sahihi. Yanaporomoka pia kwa sababu upinzani haufahamu ni mpango gani hasa wanaweza kuuwasilisha kwa wananchi, mbali na suluhisho la kauli mbiu ya " Urusi bila ya Putin". Serikali ya Urusi ingeweza kutoa haki ya waandamanaji kukusanyika. Ingeweza kujisikia vizuri, kwa kuwa rais wa Urusi anaungwa mkono kwa asilimia 80 na wananchi. Lakini haifanyi hivyo , kwa kuwa asilimia hii 80 kwa kweli ni matunda ya vitisho, ambavyo vimeendelea kwa matumizi ya nguvu kubwa."
Nae mhariri wa gazeti la Fränkischer Tag , la mjini Bamberg anazungumzia kauli ya rais wa Marekani Donald Trump kuhusu kejeli alizofanya rais huyo kwa mauaji ya kigaidi nchini Ufaransa. Mhariri anaandika:
"Rais wa 45 nchini Marekani Donald Trump kwa mara nyingine tena ametumia maneno ya kejeli alipokuwa katika mkutano na chama cha wamiliki silaha chenye ushawishi mkubwa nchini Marekani na ambacho kilichangia kiasi cha dola milioni 30 katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Marekani. Rais ambaye anaweza kununuliwa. Rais ambaye ana damu katika mikono yake."
Hayo ni baadhi ya maoni ya wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani , kama yalivyokusanywa na Sekione Kitojo:
Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman