Magazetini: Israel na Saudi Arabia na Puigdemont
4 Aprili 2018Tukianza na mada kuhusu kukaribiana kati ya Israel na Saudi Arabia baada ya mwanamfalme Mohammed bin Salman kusema kwamba Israel inahaki ya kuishi kama taifa , mhariri wa gazeti la Reutlinger General-Anzeiger anaandika:
Kwa upande wa kijeshi na mashirika ya ujasusi kumekuwa na ushirikiano baina ya Israel na Saudi Arabia. Adui yao wa pamoja Iran inaliunganisha taifa hilo la kifalme la Kiarabu la kisunni na taifa hilo la Kiyahudi, licha ya kuwa hadi sasa hakuna uhusiano wa kidiplomasia kati yao. Mwanamfalme Mohammed bin Salman anaonekana kuwa ni mtu mwenye nguvu katika ufalme huo wa Saudia. Ni mshangao mkubwa , kwamba ameweza hadharani kusema kwamba Israel inahaki ya kuishi kama taifa, ikiwa pia kwasababu Saudi Arabia ndio nchi takatifu mlinzi wa Uislamu. Hatua hiyo hata hivyo inapaswa kuchukuliwa kuwa kama tahadhari kwa Wapalestina. Kuuchochea tena mzozo wake na Israel hakutaleta manufaa, kwa kuwa uhusiano wa kimkakati kati ya Tel Aviv na Riadh una jukumu kubwa la maamuzi.
Mhariri wa gazeti la Badisches Tagblatt la mjini Baden-Baden akiandika kuhusu mada hiyo anasema:
Mwanamfalme Mohammed amechagua njia ya siasa makini na kujitoa kutoka kupuuzia kile ambacho hadi sasa kimekuwa hali halisi duniani. Anataka mkataba wa amani na taifa la Israel, ambao hadi hivi karibuni haukuwapo nchini humo, na Saudi Arabia hivi sasa inaunga mkono mapambano dhidi ya Iran, lakini pia kwa matumaini ya kiuchumi. Saudi Arabia inabakia hata hivyo mtetezi wa suluhisho la mataifa mawili katika mzozo kati ya waisrael na Wapalestina. Juhudi za hivi karibuni za kupata makubaliano ya amani zina muelekeo wa uwezekano kwa kiasi fulani. Mkaribio huu kati ya Israel na Saudi Arabia ni fursa inayofaa kuchukuliwa.
Mahakama imeamua rais wa zamani wa jimbo la Catalonia nchini Uhispania Carles Puigdemont arejeshwe nchini mwake kwa mashitaka baada ya kukamatwa nchini Ujerumani. Mhariri wa gazeti la Suedwest Presse la mjini Ulm anaandika:
Mahakama imekwisha tamka, lakini mtazamo wa msingi wa uamuzi wa mwendesha mashitaka ni kwamba kuna mwelekeo wa uhalifu katika uasi uliotokea nchini Uhispania na kufananishwa na uhaini. Hali inaonekana kwamba Carles Puigdemont atarejeshwa nchini mwake Uhispania na ambako anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 30 jela. Inaonekana sheria hii kuwa ni kali kwa wale wote wanaounga mkono uasi huo. Mafanikio ya jimbo hilo kujitenga yangekuwa kioo cha majimbo mengine , ambayo yangependa leo na sio kesho kusitishwa hali ya kuutukuza Umoja wa Ulaya.
Gazeti la Mannheimer Morgen likizungumzia kuhusu mkutano wa kilele wa viongozi wa Urusi, Uturuki na Iran kuhusu Syria linaandika:
Si Putin ama Erdogan wangependa kuachia misimamo yao kuhusiana na udhibiti wa Syria na utawala wake. Mkutano mjini Ankara , kama ilivyokuwa katika mkutano uliopita kati ya nchi hizo mjini Sochi karibu miezi mitano iliyopita, ni mfumo mwingine , wa kupata suluhisho la amani nchini Syria. Hakuna zaidi.
Hayo ni baadhi ya maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani , kama yalivyokusanywa na Sekione Kitojo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman