Magazetini: Papa Francis; Utoaji mimba ni sawa na kuuwa
11 Oktoba 2018
Mhariri wa gazeti la Mittelbayerische Zeitung la mjini Regensburg akizungumzia kuhusu uchaguzi wa jimbo la Bavaria , anaandika kwamba , kitu kinachoshangaza ni kwamba chama cha CSU kinachoongoza jimbo hilo hakijielekezi kuiangalia kwa makini siku ya uchaguzi, kuweza kujipanga kupata wingi wa kutosha kuweza kushikilia uongozi wa jimbo hilo, badala yake viongozi wanalumbana na kutupiana lawama , hususan mwenyekiti wa chama hicho na waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer kuwa ndiye anayesababisha chama hicho kushindwa. Mhariri anaandika.
Kutokana na malumbano juu ya ilani ya sera ya uchaguzi ya chama hicho , suluhisho bila shaka liko wazi. Tatizo la chama cha CSU limefika mbali zaidi. Hata suala kumhusu katibu mkuu wa chama Markus Soeder, linapaswa katika muktadha huu kuulizwa, hata kama anauungwaji mkono mkubwa ndani ya chama hicho. Kwa nini mgombea mkuu katika uchaguzi awe hahusiki katika matokeo ya uchaguzi ?
Mhariri wa gazeti la Rhein-Zeitung la mjini Koblenz akiandika kuhusiana na uchaguzi huo wa jimbo la Bavaria anasema:
Siku ya Jumapili itakuwa tu mwanzo wa wa chama cha CSU kukaribia kupoteza , mamlaka yake katika jimbo hilo. Na pia ni hatua ya kufikia mwisho kwa shughuli za kisiasa za baadhi ya viongozi. Uchaguzi wa jimbo hilo ambalo kimsingi lilikuwa linaongozwa na chama hicho, hautaamuliwa na kingine isipokuwa uongozi wa kiimla na siasa za kijinga.
Baada ya kiongozi wa kanisa Katoliki kusema kwamba utoaji mimba ni sawa na kumlipa mtu kufanya mauaji, gazeti la Badische Zeitung la mjini Freiburg limemkosoa sana kiongozi huyo wa kidini kwa kuandika:
Ni nini alichokuwa akilenga kiongozi huyo mkuu wa kanisa Katoliki kwa matamshi kama hayo na alikuwa akiwalenga watu gani ? Bila shaka sio wanawake ambao wanajiweza ambao wanaamua kwamba hawataki watoto. Pia si binadamu , ambao wanataka kuwasaidia wanawake ambao wako katika hatari ya kupoteza maisha. Papa anawaweka wanawake hawa katika hali ya unyanyapaa, na kama kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki hatambui kwamba amewaweka katika hali ngumu ya kimaisha wanawake hawa. Hata katika uongozi wa papa Francis , kanisa limejitenga, na kujijengea ukuta.
Nalo gazeti la Allgemeine Zeitung la mjini Mainz likizungumzia matamshi hayo ya papa Francis , limeandika:
Papa huwa hakosei. Lakini hapa sio tu kwamba Papa amefanya makosa makubwa, lakini kuna mengi zaidi: Amejitwika mzigo mkubwa sana. Amefanya madhambi. Kufananisha utoaji wa mimba na kumlipa mtu kufanya mauaji, amekwenda mbali mno. Ni udhalilishaji wa hali ya juu, kusababisha mgogoro mkubwa inapotokea mtu akiamua kutoa mimba.
Mada ya mwisho ni kuhusu mfumko wa bei , ama ughali wa maisha nchini Uturuki. Mhariri wa gazeti la Stuttgarter Nachrichten anaandika:
Hatua za hivi karibuni zilizochukuliwa na serikali ya Uturuki kupambana na ughali wa maisha unaopindukia mipaka ni ishara kwamba , serikali ya nchi hiyo inataka kufanya kila inaloweza kuchukua hatua kali zaidi. Kuwaweka wakaguzi wa udhibiti wa bei kuchunguza bei katika maduka ya vyakula nchini humo si mkakati sahihi wa sera za kiuchumi. Serikali ya Erdogan inatapatapa tu. Kwa njia hiyo haiwezi kurejesha imani ya wawekezaji. Hata waungaji wake mkono wanaanza kulalamika. Erdogan aliahidi katika kampeni za uchaguzi kwamba hali itaimarika, lakini hadi sasa ni mtafaruku mtupu na kupanda kwa bei.
Hayo ndio machache ambayo Sekione Kitojo ameweza kutuchambulia kutoka kwa wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu