Magazetini: Merkel ziarani katika bara la Afrika
30 Agosti 2018Tukianza na gazeti la Markische Oderzeitung la mjini Ftrankfurt , mhariri anaadika kwamba kansela anafanya ziara nchini Senegal, Ghana na Nigeria. Mhariri anaendelea:
"Wakati huo huo waziri wa ushirikiano wa maendeleo Gerd Mueller anafanya ziara katika mataifa mengine ya Afrika. Bila shaka, Ujerumani imekuwa wakati wote ikilitupia jicho bara la Afrika. Katika kupambana na masuala ya wakimbizi, kuhusu mahitaji ya maendeleo na uwezekano wa uwekezaji hususan kwa makampuni ya Ujerumani. Haya yote ni mambo mazuri na sahihi. Bora zaidi lakini , ingekuwa sahihi, iwapo kungekuwa na mkakati maalum wa utendaji wa hayo yote. Kwa kuwa hilo bado halieleweki."
Kuhusiana na mada ya enzi za utawala wa kikoloni nchini Namibia , mhariri wa gazeti la Nuernberger Nachrichten , anaandika kwamba, vinyago , mapambo na vifaa vya sanaa kutoka katika mataifa ya Afrika mara nyingi sio kwamba vimekuwapo tu katika majumba ya makumbusho ya Ulaya, lakini kwa kiasi kikubwa vinafungamanishwa na historia ya ukoloni. Mhariri anaandika:
"Na mara nyingi ni kama uporaji wa sanaa. Na historia ya ukoloni wa Ujerumani kwa kweli si ya muda mrefu , ilidumu si zaidi ya miongo mitatu na kumalizika mwaka 1918 kwa kushindwa kwa Ujerumani katika vita vikuu vya kwanza vya dunia. Matokeo yake lakini yanaonekana hadi hii leo. Mada hii lakini inapaswa kuangaliwa kwa undani kwa kuwa Ujerumani ni nchi ambayo ina wahamiaji wengi hivi sasa. Watu kutoka bara la Afrika ama mashariki ya kati hivi karibuni ama baadaye watatuuliza maswali kuhusu urithi wao wa kiutamaduni. Hii haihusiani na suala la kurejesha vitu vyote vilivyokusanywa kutoka katika enzi za ukoloni. Lakini ni lazima kuwe na mjadala wenye usawa pamoja na mataifa haya ambayo sanaa hizi zimechukuliwa, kuhusu nini kilitokea wakati wa uporaji wa urithi huu wa utamaduni."
Mhariri wa gazeti la Hessische Niedersaechsische Allgemeine la mjini Kassel , akizungumzia kuhusu mada hiyo ya enzi za utawala wa kikoloni wa Ujerumani nchini Namibia anaandika:
"Hatua nyingine ni lazima ichukuliwe. Ni lazima kuomba rasmi samahani ambayo hadi sasa bado suala hilo halijafanyika. Ni enzi za aibu. Haitakuwa vizuri kwa kuchukua hatua nzuri tu. Serikali ya Ujerumani haioni sababu yoyote ya msingi kwa madai ya Namibia ya kupatiwa fidia ama kwa watu mmoja mmoja wa kabila la Herero na Wanama. Lakini kuna ulazima wa takriban kufikiwa makubaliano juu ya kupatiwa msaada makabila hayo mawili."
Kuhusiana na mada juu ya tathmini ya kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew kwa kutolewa na mapema timu ya taifa katika fainlai za kombe la dunia nchini Urusi mwaka huu, mhariri wa gazeti la Mitteldeutsche Zeitung la mjini Halle anaandika:
"Kutokana na matatizo mengi , wakati wa fainali za kombe la dunia na katika timu ya taifa , ni wazi kwamba mambo haya yanatofautiana, na kwamba kocha Loew pamoja na mkurugenzi wake wa soka Oliver Bierhof wameyaelewa kidogo ama hawajayaelewa kabisa. Hilo limeonekana katika tathmini. Huo si mwanzo mpya, badala yake ni ushuhuda wa kushindwa."
Mwandishi: Sekione Kitojo / ilandspresse
Mahriri: Mohammed Khelef