1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani yazungumzia mpango wa kuinusuru Sudan

16 Juni 2023

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha na mgogoro unaoendelea nchini Sudan, kuuliwa kwa wahanga wa vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na machafuko nchini Senegal pamoja na mambo mengine.

https://p.dw.com/p/4SgpW
Sudan West Darfur | Geneina
Picha: Str/AFP

Gazeti la der Tagesspiegel ambalo liliandika kuhusu "Mpango wa kuinusuru Sudan". Nchi jirani zinataka kupatanisha. Mapigano ya barabarani, milipuko na mashambulizi ya mabomu kutokea angani yameuharibu mji mkuu wa Sudan, Khartoum. Mamia kwa maelfu ya watu wanakimbia. Tangu mzozo kati ya jeshi la Sudan na waasi, hali imeendelea kuwa tete Sudan. Mhariri ameandika kwamba katika jimbo la Darfur, magharibi mwa nchi waasi wa kikabila pia wameingilia kati, hali inayoongeza hofu kwamba mapigano huenda yakasambaa zaidi na kudumu muda mrefu.

Mgogoro wa Sudan kusambaa Darfur

"Wakati mashetani walipokuja wakiwa juu ya farasi". Ndivyo alivyoandika Issio Ehrich mwandishi wa gazeti la Die Zeit kuhusu vita vinavyoendelea nchini Sudan. Vita kati ya majenerali wawili wa Sudan vinachochea mgogoro wa zamani wa kikabila katika jimbo la Darfur, magharibi mwa nchi hiyo. Kadri Saddam Mohammed Ahmed anavyoweza kukumbuka, dada yake mkubwa alifanya kazi katika bustani yake katika mji alikozaliwa wa Tendelti, magharibi ya Sudan. Alipenda sana kupanda mbegu kwenye mchanga wenye rangi nyekundu na maji ya kunde. Miezi michache baadaye alikuwa akivuna nyanya, mrenda na vitunguu.

Mwandishi anaeleza kwamba asubuhi ya Mei 17, wanaume waliingia mjini Tendelti wakiwa juu ya farasi. Walikuwa na bunduki za rashasha, mashine za kuvurumishia maroketi na maguruneti. Ahmed anasema walikuwa ni wapiganaji wa Janjaweed - mashetani juu ya farasi. Wanaume hao wanaoelezwa na watu walioshuhudia kama watu weupe, waliwapiga risasi wakazi Waafrika na kuzichoma nyumba zao. Uvamizi huo ulidumu kwa saa kadhaa. Risasi moja ikampata dada yake Ahmed katika moyo wake. Aliuwawa kwenye kishamba chake kidogo kwenye bustani. Gazeti linasema katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan, mzozo uliochochewa kikabila ambao ulizigubika hisia za ulimwengu kiasi miaka 20 iliyopita unatokota tena.

Wakimbizi wa ndani wauliwa Congo

Watu waliolazimika kuyahama makazi yao wauwawa kiholela Congo. Ndivyo lilivyoandika gazeti la die Tageszeitung. Uvamizi uliofanywa na kundi la waasi mkoani Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Hema ulisababisha vifo vya watu 46. Mwandishi wa gazeti la die Tageszeitung Dominic Johnson amesema wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa walikuwa kilometa chache kutoka eneo hilo lakini hawakuingilia kati.

DR Kongo Rethy | militante Milizgruppe URDPC/CODECO
Makomando wa kundi la waasi la CODECOPicha: ALEXIS HUGUET/AFP

Baadhi ya picha zinaonesha vijumba vya nyasi vikiteketea, nyingine zinaonesha maiti zilizoteketea kabisa kwa moto, nyingine za watoto wadogo sana. Watoto 24 wanaaminiwa kuwa miongoni mwa watu 46 waliouliwa katika uvamizi uliofanywa na kundi la waasi wa CODECO katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Lala katika jimbo la Ituri Jumatatu usiku. Yanaelezwa kuwa mauaji mabaya kabisa kufanywa katika kambi ya wakimbizi nchini Congo katika kipindi cha miongo kadhaa.

Vijana wa Senegal wampinga rais Macky Sall

Gazeti la mtandaoni la Zeit Online liliandika kuhusu yanayoendelea nchini Senegal. Vuguvugu la vijana lilimsadia rais Macky Sall kuingia madarakani. Sasa vijana wa Senegal wanamuwekea vizuizi na kumpinga rais huyo. Je ni ishara ya kuelezea hisia zao kuhusu demokrasia muhimu inayohitajika au ni machafuko tu ya kawaida? Aliandika na kuuliza Andrea Böhm, mwandishi wa taarifa hiyo. Vijana wamechoshwa na mzunguko wa migogoro inayotokea kwa kasi zaidi katika bara la Afrika kuliko bara jirani la Ulaya. Vita, viongozi wa kiimla, na ufisadi ni mada zinazoandikwa mara kwa mara katika sehemu ya gazeti la Zeit Online kuhusu nchi za kiafrika.

Mwandishi alisema migogoro hupuuzwa mara kwa mara katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na hata pia mitazamo hasi kuhusu madhila ya muda mrefu ya bara la Afrika. Senegal imepata umaarufu katika siku za hivi karibuni kwa sababu kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameahidi kumuunga mkono rais wa Senegal Macky Sall katika utafutaji wa gesi asilia nje ya pwani ya Senegal kwa lengo la kuhakikisha usalama wa upatikanaji wa nishati Ujerumani. Mwandishi anasema kufikia sasa hali ni mbaya, angalau katika mtazamo wa sera ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mali yaandaa kura ya maoni kuhusu katiba mpya

Gazeti la Die Tageszeitung lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema "Kiongozi wa kijeshi wa Mali kuwa na katiba mpya hivi karibuni". Kura ya maoni ya katiba Jumapili inatarajiwa kufungua mlango kwa kiongozi wa mapinduzi Assimi Goita kuchaguliwa kuwa rais na hatimaye Umoja wa Mataifa utaweza kuondoka pia. Mwandishi wa gazeti la Der Tagespiegel Dominic Johnson ameandika kwamba Assimi Goita kwa sasa uwepo wake uko kila mahali nchini Mali. Kanali huyo aliyeandaa mapinduzi mnamo 2020 na kujitangaza mwenyewe kuwa rais mwaka 2021, anahimiza kura ya ndio wakati raia wa Mali wanapoipigia kura katiba mpya leo Jumapili.

Mali Präsident Oberst Assimi Goita
Assimi GoitaPicha: Habib Kouyate/Xinhua/IMAGO

Katiba hiyo inanuiwa kufungua njia kwa kurejesha demokrasia nchini Mali kufuatia mapinduzi ya mwaka 2020 na 2021. Kwa mujibu wa katiba hiyo uchaguzi unatarajiwa kuandaliwa Februari 2024 ili rais aliyechaguliwa kwa njia ya kura aiongoze tena nchi hiyo. Mwandishi wa gazeti la der Tagesspiegel anasema uwezekano kwamba rais atakuwa Assimi Goita ni mkubwa. Katiba inayopigiwa kura inamruhusu kugombea wadhifa wa urais na unaimarisha mamlaka ya ofisi ya rais ambayo tayari ni makubwa.

Gavana wa benki kuu Nigeria atimuliwa

Mtaalamu wa benki wa haiba kubwa atolewa kafara kwa vurugu za rushwa Nigeria. Rais mpya wa Nigeria Bola Tinubu anataka kusafisha uchumi wa nchi uliogubikwa na rushwa na ameanza kwa kumtupa gerezani gavana wa benki kuu Godwin Emefiele. Mwandishi wa gazeti la die Tageszeitung Emeka Okonkwo anasema miezi michache iliyopita Godwin Emefiele alikuwa mmojawapo wa wanaume wenye mamlaka na nguvu kubwa Nigeria, kama sio barani Afrika. Aliongoza benki kuu ya nchi yenye uchumi mkubwa Afrika na alitaka kuwa rais. Leo, mtaalamu huyo wa benki mwenye umri wa miaka 61 yuko gerezani.

Emefiele ni muhanga wa kwanza mashuhuri wa rais mpya wa Nigeria, Bola Tinubu, aliyeingia madarakani Mei 29, akiahidi kuufagia na kuutokomeza ufisadi na usimamizi mbovu wa uchumi. Emefiele alitimuliwa Ijumaa iliyopita na kuamriwa akabidhi afisi kwa naibu wake Folashodun Adebisi Shonubi. Msemaji wa serikali ya Nigeria Willie Bassey alinukuliwa na gazeti la die Tageszeitung akisema hatua hiyo ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea na pia mipango ya mageuzi katika sekta ya fedha iliyoandaliwa. Kukamatwa kwa Emefiele kumeibua utata huku tetesi za kutiwa mbaroni zikianza kuzagaa Jumamosi wiki iliyopita.

(Inlandspresse)