Magazeti ya Ujerumani yaandika juu ya Mali,Boko Haram na hatari ya mitumba
19 Februari 2012Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linakumbusha juu ya mauaji halaiki yaliyofanywa na waasi wa Wakitaureg wanaopigania kujitenga kaskazini mwa Mali. Gazeti hilo linatilia maanani katika makala yake kwamba waasi hao wamewaua askari wa jeshi la Mali pamoja na raia.Askari hao walikuwa mateka.
Katika makala yake gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaarifu kwamba chama cha waasi wa Kitaureg kinachoitwa "Movement for the Liberation of Azawad",kinapigania "uhuru" wa jimbo la Azawad, kaskazini mwa Mali.
Gazeti la "Frankfuter Allgemeine" limeikariri taarifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu inayosema kuwa watu karibu 30,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mapigano kaskazini mwa Mali. Shirika la Msalaba mwekundu pia limearifu kwamba maalfu ya watu wengine wamekimbilia katika nchi jirani.
Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" wiki hii pia limeandika juu ya makubaliano ya kumaliza mvutano baina ya Sudan na Sudan ya Kusini.Mapatano hayo yalifikiwa mjini Addis Ababa mwishoni mwa wiki iliyopita. Nchi hizo zimekubaliana juu ya mkataba wa kutoshambuliana.
Kwa mujibu wa mkataba huo Sudan na Sudan ya Kusini zimejiwajibisha kuheshimu himaya ya kila upande, kutojingiza katika mambo ya ndani ya upande mwingine na kuyatatua matatizo yote kwa njia ya mazungumzo. Gazeti la "die tageszeitung" wiki hii limechapisha makala juu ya kundi la wanaitikadi kali wa kiislamu, Boko Haram la nchini Nigeria. Gazeti hilo limeandika kwamba mashambulio ya kigaidi yanayofanywa na kundi la Boko Haram yanawanufaisha matajiri, wakati ambapo Nigeria inakabiliwa na mfarakano mkubwa wa kijamii.
Gazeti la hilo linatilia maanani kwamba kundi la Boko Haram linaweza kuwavutia watu fulani kutokana na sababu za kiuchumi. Gazeti la"die tageszeitung" linasema licha ya Nigeria kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika uuzaji wa mafuta duniani, wananchi Milioni 100 wa nchi hiyo wanaishi kwa kipato cha chini ya Euro moja kwa siku. Gazeti la "die tageszeitung" linasema mazingira hayo ni rutuba inayolistawisha kundi la Boko Haram.
Gazeti la "Financial Times Deutschland" "pia limeandika juu ya matukio ya nchini Nigeria. Lakini gazeti hilo linaizingatia sekta ya uchumi. Linasema ubepari unastawi nchini Nigeria, na linaeleza kwamba licha ya taarifa za kutisha juu ya umaskini na njaa,bara la Afrika linastawi. Watu wake ni vijana na ni wanunuzi wazuri.Gazeti hilo linasema serikali za Afrika zinazifuata taratibu za uchumi wa soko. Gazeti la "Financial Times Deutschland" linakumbusha kwamba baada ya kujitenga na dunia mnamo miaka ya 90 hadi 2008, bara la Afrika sasa linaziba pengo haraka.
Gazeti hilo limelizinukuu takwimu za Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, zinazoonyesha kwamba mnamo mwaka huu bara la Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara, litastawi kwa wastani wa asilimia 5 .5.
Gazeti la "Neues Deutschland" wiki hii linatahadharisha juu ya hatari ya biashara ya mitumba ya kieletroniki inayoingia barani Afrika kutoka Ulaya. Mitumba hiyo ni pamoja na mafriji,kompyuta,simu, televisheni na hata mashine za kufulia. Gazeti la "Neues Deutschland" linasema biashara hiyo inastawi barani Afrika. Limezinukuu taarifa za mashirika ya Umoja wa Mataifa zinazoonyesha kwamba tani 230,000 za mitumba ya mafriji,kompyuta na televisheni zimeingia magharibi mwa Afrika kuanzia mwaka wa 2009.
Gazeti la "Neues Deutchland" limearifu kwamba mitumba hiyo inauzwa hasa,Ghana,Liberia,Nigeria na Benin. Katika miji ya Lagos na Accra watu 30,000 wanaitegemea biashara ya mitumba hiyo. Lakini gazeti hilo linasema hakuna anaeweza kuzungumzia juu ya mafanikio ya biashara hiyo.
Mitumba hiyo inasababisha maradhi. Vitu hivyo ni hatari kwa sababu vinatokana na mchanganyiko wa madawa mengi vinapotengenezwa. Wanaohatarishwa na mitumba hiyo hasa ni watoto wanaotembea bila ya viatu wanapotafuta vitu kwenye majaa ya mitumba hiyo yenye sumu.
Mwandishi: Mtullya Abdu
Deutsche Zeitungen:
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman