Magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika
9 Februari 2024Frankfurter Allgemeine
Mhariri ameandika kwamba uchaguzi wa rais nchini Senegal ulipangwa kufanyika mwishoni mwa Februari sasa umeakhirishwa hadi mwezi Desemba.Baada ya majadiliano makali kwenye bunge la nchi hiyo mjini Dakar,ulifikiwa uamuzi wa kuunga mkono kuakhirishwa uchaguzi huo.Pendekezo lililotolewa mwanzo,ni kuufanya uchaguzi huo baada ya miezi sita ijayo lakini baadae ikaonekana kwamba kipindi hicho shule zitakuwa zimefungwa na utakuwa vile vile msimu wa mvua na kwahivyo ukasukumwa mpaka mwezi Desemba.Mjini Dakar zilishuhudiwa vurugu Jumanne kufuatia maandamano yaliyochochewa na uamuzi huo.Ikumbukwe ni mara ya kwanza kwa Senegal kuakhirisha uchaguzi.Mhariri wa frankfurter Allgemeine anasema bado yapo maswali mengi ambayo hayajapatiwa ufumbuzi.Watu wanajiuliza je rais Macky Sall anaweza kuendelea kubakia madarakani muhula wake utakapomalizika Aprili 2?Mhaririri huyo pia anasema umma wa Wasenegal umeshapoteza imani na taasisi zao ikiwemo baraza la katiba,bunge na mahakama.
Gazeti la die tageszeitung
Wapinzani na wakosoaji wa serikali wanaamini rais Macky Sall ni wazi sasa ataendelea kubakia madarakani, pengine kwa takriban mwaka mmoja zaidi.Wakati mwanzoni ilifikiriwa uchaguzi huo ungeakhirishwa kwa miezi sita,umesogozwa hadi mwezi Desemba.Maana yake ni kwamba Rais Macky Sall atabaki madarakani mpaka atakapopatikana mrithi wake.Mhariri anasema,na ikiwa uchaguzi huo wa Desemba utalazimika kwenda kwenye duru ya pili,hapana shaka duru hiyo ya marudio italazimika kufanyika mwishoni mwa mwezi Januari na pengine hata mwanzoni mwa Februari mwaka ujao.Wapinzani wanamtaka rais Macky Sall ajiuzulu wakisema kilichofanyika sio demokrasia.Mhariri anakumbusha kwamba kuna wanasiasa kadhaa wa upinzani,akiwemo kiongozi wa chama kikuu cha Upinzani Ousmane Sonko wako jela.
Süddeutsche Zeitung
Demokrasia ya Senegal inaporomoka.Rais Macky Sall ameuakhirisha uchaguzi na kuitumbukiza nchi yake katika mgogoro.Mhariri anaongeza kusema, Macky Sall ameyafanya yote hayo licha ya kushuhudiwa matatizo chungunzima na mapinduzi katika kanda ya Afrika Magharibi.Lakini Muhariri hapo hapo anasema,si haba tarehe ya kufanyika uchaguzi imetangazwa,Japo haimaanishi kwamba hatua hiyo itayafanya mambo kuwa bora. Uchaguzi wa Senegal utafanyika Desemba tarehe 15 kama lilivyoamuwa bunge la nchi hiyo ya Afrika Magharibi, mnamo siku ya Jumatatu.Mhariri anasema sasa Senegal imeshatumbukia kwenye mgogoro uliosababishwa na Macky Sall ambaye hapana shaka ataendelea kubakia madarakani.Anasema Kanda ya Afrika Magharibi inakabiliwa na kipindi cha dhoruba,kuanzia ugaidi,mabadiliko ya tabia nchi mpaka ukosefu wa uthabiti wa kisiasa.Kanda hiyo inakabiliwa na wimbi la mapinduzi zikiwemo nchi jirani na Senegal za Mali na Guinea zinazoshikiliwa na tawala za kijeshi.Mhariri huyo anakumbusha kwamba Senegal imekuwa nchi inayojivunia kuwa na utulivu na uthabiti wa kuachiana madaraka kwa njia ya amani.Haijawahi kushuhudia mapinduzi.Lakini nchi hiyo ya wakaazi milioni 17 inapoteza kwa kasi hadhi hiyo.
Frankfurter Allgemeine Zeitung
Mahakama moja ya Kenya imemfungulia mashtaka kiongozi wa madhehebu iliyowalazimisha wafuasi kuacha kula na kunywa,na washukiwa wengine kadhaa kwa matukio 191 ya mauaji.Paul Nthenge Mackenzie na washukiwa wengine 29 walikanusha mashataka yote.Kesi hiyo inahusina na kugundulika kwa makaburi ya watu wengi mnamo mwezi Aprili mwaka 2023 katika msitu wa Shakahola huko nchini Kenya ambako mabaki ya watu 429 yalifukuliwa.Kisa hiki kiliitikisa sana nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Soma pia: Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii
Neue Zürcher Zeitung ameitazama michezo ya AFCON
Kufumba na kufumbua wenyeji wa michuano hiyo,Ivory Coast wameonesha maajabu.Pale walipoonekana sio mara moja wala mara mbili kwamba watayaaga mashindano hayo,wameendelea kuwashangaza mashabiki wa soka na kuonekana kwamba huenda inawezekana pia kwa kocha wao mpya Olaf Jansen kuifanikisha timu hiyo kuunyakuwa ubingwa.Mhariri huyo ameitazama kwanza mechi ya robo Fainali kati ya timu hiyo dhidi ya Mali,na kusema,ama kwahakika,Bouake,Uwanja wa amani,ulitikisika.Shangwe kubwa liliufunika uwanja huo pale mchezaji mchanga Oumar Diakité alipoifungia Ivory Coast sekunde za mwisho kabisa za dakika za ziada na kuipatia ushindi wa mabao 2 kwa 1 dhidi ya Mali.Lakini maajabu ya timu hiyo hayakuishia hapo .Shangwe likatawala tena walipopata ushindi kwenye nusu Fainali dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuicharaza bao 1-0.Na kwa mara ya kwanza watakutana kwenye Fainali ya michuano hiyo Jumapili dhidi ya Super Eagles Nigeria walioingia baada ya kuilaza Afrika Kusini kupitia mikwaju ya Penalti.Mhariri anasema hakuna mgahawa au hoteli inayokosa televisheni kubwa kuonesha shangwe la ushindi wa timu hiyo,katika michuano iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa kufanyika katika taifa hilo ambalo limeshuhudia migogoro ya vita vya wenyewe kwa wenyewe hadi mwaka 2011.