Magaidi wavamia hoteli Ouagadougou
16 Januari 2016Kwa mujibu wa taarifa watu wasiopungua 20 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika tukio hilo. Mkurugenzi wa hospitali amethibitisha kuwa miongoni mwa waliouawa walikuwa raia 14 wa nje.
Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema magaidi hao waliivamia Hoteli hiyo na kuanza kuyachoma moto magari yaliyokuwa nje huku wakifyatua risasi hewani ili kuyatawanya makundi ya watu kabla ya kuwasili kwa vikosi vya usalama.
Ubalozi wa Ufaransa nchini Burkina Faso umesema shambulio hilo ni la kigaidi, na kundi lenye uhusiano na mtandao wa Al- Qaeda limedai kuhusika.
Makomando walijitosa ndani ya hoteli hiyo saa chache baada ya kuvamiwa na magadi. Wizara ya ulinzi ya Marekani imefahamisha kwamba afisa mmoja wa jeshi la nchi hiyo alikuwa anatoa ushauri kwa makomando wa Burkina.
Hapo awali palikuwa na taarifa juu ya kutekwa watu kadhaa na kuzuiliwa ndani ya hoteli. Moto mkubwa ulizuka baada ya magaidi waliokuwa na silaha kuivamia hoteli ya Splendid. Lakini majeshi ya usalama yaliwasili muda mfupi tu baadae na kuanza kupambana na magaidi.
Amri ya kutotoka nje kuanzia usiku wa manane hadi saa 12 asubuhi yatangazwa
Balozi wa Ufaransa nchini Burkina Faso ,Gilles Thibault amethibitisha kutangazwa amri hiyo.Kulingana na takwimu za wizara ya mambo ya ndani, Wafaransa zaidi ya 3500 wanaishi nchini Burkina Faso.
Hapo awali palikuwapo habari juu ya uwezekano wa majeshi ya Ufaransa kushiriki katika juhudi za kuikomboa hoteli ya Splendi. Hata hivyo balozi Gilles Thibault hajathibitisha habari hizo. Wanajeshi wa Ufaransa wana kambi ya kudumu nchini Burkina Faso.
Tawi la Al-Qaeda magharibi mwa Afrika,AQIM limedai kupanga mashambulio hayo. Kundi hilo limekaririwa likisema katika lugha ya kiarabu kwamba wapiganaji wake wanapambana na maadui wa dini ya Kiislamu.
Burkina Faso ambayo ni nchi yenye waumini wengi wa dini ya kiisilamu imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa kisiasa tangu Oktoba 2014 yalipofanyika maandamano yaliyolazimisha kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Blaise Compaore ambapo pia imekuwa ikiandamwa na mashambulizi yanayodaiwa kupangwa na wapiganaji wa makundi ya itikadi kali.
Watu wa Burkina Faso hivi karibuni walipiga kura kumchagua Rais mpya mwaka mmoja baada ya kumtimua Blaise Compaore. Mamilioni walishiriki katika uchaguzi uliozingatiwa kuwa kidemokrasia kuwahi kufanyika katika historia ya nchi hiyo ya Afrika magharibi.
Mwandishi: Abdul Mtullya
Mhariri : Isaac Gamba