1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yazidi kuitesa Uingereza

13 Februari 2014

Upepo mkali unaovuma kutoka Bahari ya Atlantiki umewakatia umeme maelfu ya raia wa Uingereza, ukiongeza fadhaa ya balaa kubwa kabisa la mafuriko kuiwahi kuikumba nchi hiyo kwa miaka 250.

https://p.dw.com/p/1B82Z
Matrekta yakitumika kuziokoa gari zilizonasa kwenye mafuriko.
Matrekta yakitumika kuziokoa gari zilizonasa kwenye mafuriko.Picha: picture alliance/dpa

Kufika sasa, nyumba zipatazo elfu thamanini hazina umeme, huku Wales ikiwa imeathirika zaidi na upepo uliopewa jina la "Wild Wednesday".

Upepo huo unaokwenda kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa, umepiga maeneo kadhaa ya England na Wales, huku Mto Thames ulio karibu na London ukijaa katika kiwango ambacho hakijawahi kutokea kwa zaidi ya miaka 60 iliyopita.

Mtu mmoja anaripotiwa kufa baada ya kunaswa na umeme pale alipojaribu kuundosha mti uliovunja nguzo ya umeme mjini Wiltshire, kusini magharibi mwa England. Huyu ndiye mtu wa kwanza kupoteza maisha kwenye janga hili.

Hali mbaya ya hewa ilisababisha pia mtafaruku kwenye usafiri wa umma, huku treni na mabasi ya abiria yakikwama mjini Yorkshire, kaskazini mwa England.

Athari za mafuriko

Tayari Idara ya Hali ya Hewa imeshatoa onyo lenye alama za juu, ikimaanisha kwamba kutakuwa na pepo kali zaidi katika maeneo ya magharibi mwa Wales na kaskazini magharibi mwa England.

Helikopta ikifanya kazi ya uokozi kwa waathirika wa janga la mafuriko.
Helikopta ikifanya kazi ya uokozi kwa waathirika wa janga la mafuriko.Picha: picture alliance/dpa

Tim Field wa Jumuiya ya Mashirika ya Nishati ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wanafanya kila wawezalo kurudisha huduma ya umeme kwenye maeneo hayo.

Gavana wa Benki ya England, Mark Carney, amesema hatua za Uingereza kujijenga upya kutoka mserereko wa kiuchumi zinaweza kuathiriwa sana na hali hii mbaya ya hewa, ambayo imeharibu mashamba na miundombinu ya usafirishaji.

Maafisa wa serikali wanasema, zaidi ya nyumba 5,800 zimeshaghariki tangu mafuriko yalipoanza mwezi Disemba mwaka jana kwenye mji wa kusini magharibi wa Somerset.

Tangu mwezi Januari, Mto Thames umeathiriwa vibaya na maafisa wanasema ndani ya kipindi cha wiki mbili tu zilizopita, mto huo umesababisha zaidi ya nyumba 1,100 kuzama.

Wanajeshi zaidi wamepelekwa kushiriki juhudi za uokozi na wamekuwa wakiweka magunia ya mchanga kuzunguka vijiji vilivyo hatarini kuzama, huku skuli za msingi zikigeuzwa kuwa vituo vya huduma za dharura.

Mratibu wa huduma hizo kutoka jeshi la Uingereza, Meja Jenerali Patrick Sanders, ameiita hali hiyo kuwa ni janga la kimaumbile lisilo mfano wake.

Cameron alaumiwa

Katikati ya mwezi Januari, chama kinachopinga wahamiaji nchini Uingereza, UK Independence Party (UKIP), kilimsimamisha mbunge wake mmoja aliyedai kuwa mafuriko hayo yamesababishwa na uamuzi wa serikali kuhalalisha ndoa za jinsia moja.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.Picha: Reuters/Laurent Dubrule

David Silvester, Mkristo wa siasa kali aliyejiengua kutoka chama cha Conservative cha Waziri Mkuu Cameron mwaka jana kupinga uamuzi huo, alidai Uingereza inaadhibiwa kwa kumkasirisha Mungu.

Wakati huo huo, maafisa wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, wameelezea kusikitishwa kwao na hatua ya serikali ya Uingereza kutokuomba fedha kutoka Mfuko wa Mshikamano wa Umoja huo, kukabiliana na janga hili.

Hata Ujerumani, ambayo ndiyo nchi tajiri zaidi kwenye Umoja wa Ulaya, iliomba msaada wa maelfu ya euro baada ya kukumbwa na mafuriko mwaka 2012.

Lakini hadi sasa, Umoja huo haujapokea ombi lolote kutoka serikali ya Uingereza, ambayo wazo lake la kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya huenda ukalifanya ombi kama hilo kuwa na mvuto wa kisiasa.

Waziri Cameron alitangaza juzi Jumanne kwamba fedha halitakuwa kikwazo katika kupambana na mafuriko hayo, lakini mawaziri wengine wamekiri kwamba serikali ilichelewa sana kuchukuwa hatua muafaka wakati mafuriko hayo yalipokuwa yanaanza.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman