1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yasababisha vifo vya watu 106 nchini Brazil

1 Juni 2022

Idadi ya waliokufa kutokana na mafuriko makubwa na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua za masika nchini Brazil imepanda na kufikia watu 106 huku vikosi vya uokoaji vikiendelea kuwatafuta wengine waliotoweka.

https://p.dw.com/p/4C71K
Brasilien Flut Amazonas Careiro Da Varzea
Picha: Bruno Kelly/REUTERS

Idadi hiyo imeendelea kupanda baada ya kupatikana kwa miili ya watu wengine iliyofukiwa kwenye vifusi vya majengo yaliyoharibiwa na mafuriko ambayo yamelikumba eneo la Kaskazini Mashariki mwa Brazil.

Walionusurika wamelifananisha janga hilo na Tsunami kutokana na uharibifu mkubwa ulioshuhudiwa hususan kwenye jimbo la Pernambuco ambako karibu wilaya 24  zimetangaza hali ya dharura kufuatia athari za mafuriko.

Maporomoko ya udongo yameharibu nyumba nyingi kwenye vitongoji kadhaa ikiwemo eneo lenye wakaazi wa kipato cha chini la Jardim Monteverde nje kidogo ya mji wa Recife ambao ni mji mkuu wa jimbo la Pernambuco.

Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa majina ya Eliane Teixira Dos Santos, alikuwa akifanya biashara ya kuuza vipodozi lakini sasa anaishi kwenye moja ya nyumba inayowahifadhi manusura wa mafuriko na amepoteza karibu kila kitu.

"Nimeishi hapa kwa miaka mingi na sijawahi kuona janga kama hilo. Hivi sasa kila mtu hana makaazi, tunalala makanisani na sote tuko hapa kwenye nyumba hii ya dharura. Jana niliamka saa 5.30 asubuhi kutoa msaada, kwa sababu inabidi tusaidiane" amesema Dos Santos.

Mwanamke mwingine Maria Heronize huku akilengwa na machozi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa amepoteza marafiki wengi na mafuriko yaliyotokea ni janga la kutisha.

Juhudi za uokozi na kutafuta waliokufa zinaendelea 

Brasilien Unwetter in Pernambuco
Juhudi za uokozi zinaendelea huko jimboni Pernambuco Picha: PERNAMBUCO STATE GOVERNMENT/AFP

Vikosi vya uokozi vinaendelea kupekua kwevye vifusi vikisaidiwa na mbwa wa polisi kuwatafuta manusura au miili ya waliofikwa na uamuti kwenye janga hilo.

Gavana wa jimbo la Pernambuco Paulo Camara ameviambia vyombo vya habari kuwa kipaumble cha serikali kwa sasa ni kuwatafuta wote ambao hawajulikani waliko kutokana na athari za mafuriko na maporomoko ya udongo. Ameapa kuwa waokoaji hawataondoka mitaani hadi wote waliopotea watakapopatikana.

Idara ya kukabiliana na majanga nchini Brazil imetahadharisha kuwa mafuriko zaidi yanaweza kuendelea kulikumba jimbo la Pernambuco hususani mji mkuu Recife. 

Mvua zinazoendelea kunyesha zilianza wiki iliyopita lakini ziliongezeka usiku wa Ijumaa na Jumamosi ya wiki hiyo na kuendelea kunyesha hadi mwanzoni mwa wiki hii.

Helikopta ya rais Bolsonaro yashindwa kutua kutokana na wingi wa maji 

Brasilien Flut Amazonas Careiro Da Varzea
Picha: Bruno Kelly/REUTERS

Hapo jana rais Jair Bolsonaro wa Brazil alilitembelea eneo hilo lakini helikopta yake ilishindwa kutua kwa sababu eneo kubwa limezingirwa na maji.  

Aliahidi baadae kuwa serikali yake itatuma msaada wote wa uokozi na kiutu unaohitajika kuwasaidia wahanga wa janga hilo.

Mafuriko ya sasa ni tukio la nne kuikumbuka Brazil ndani ya kipindi cha miezi mitano iliyopita.

Wengi wanalaumu ujenzi duni wa miundombinu kwenye maeneo ya mijini na uwepo wa makaazi holela kwenye maeneo ya miinuko kuwa chanzo cha athari kubwa pindi mafuriko au maporomoko ya udongo yanapotokea. 

Mnamo mwezi Februari watu 233 walikufa kutokana na mafuriko na maporoko ya udongo kwenye mji wa kihistoria wa Petropolis. Hapo kabla watu 28 walipoteza maisha kwenye janga la mafuriko huko Sao Paulo mwanzoni mwa mwezi Januari .