Mafuriko yaleta hatari ya kusambaa kwa magonjwa Asia ya kusini.
9 Agosti 2007Maelfu ya vijiji katika jimbo la Bihar nchini India vimekumbwa na mafuriko kwa muda wa wiki mbili zilizopita, lakini eneo moja la vijiji kadha limekuwa ndani ya maji kwa muda wa miaka 12 iliyopita. Tangu mwaka 1995, wakaazi wa Barabih ama wameendelea kuishi na mafuriko ama wameondoka.
Kiasi cha asilimia 75 ya wakaazi wameondoka na kuwaacha kiasi cha watu 1,400 tu ambao wameamua kubaki.
Zaidi ya wiki mbili za mvua kubwa katika maeneo mengi ya kaskazini mwa India, Bagladesh na Nepal yamekumbwa na mafuriko katika mito na maeneo ya uwanda , na kusababisha vifo vya watu wapatao zaidi ya 475 na watu wengine zaidi ya milioni 19 wakiwa wamekwama katika maeneo yao.
Idadi ya wahanga hadi sasa waliofariki kutokana na mvua na mafuriko hayo inazidi kupanda, na imefikia watu 2,000 na waziri mkuu Manmohan Singh leo ametoa amri ya kutoa fedha za dharura kwa ajili ya kuwapelekea misaada watu walioathirika na mafuriko hayo. Wakati kwa miaka kadha mvua hizi za majira ya Monsoon zilikuwa zikingojewa kwa hamu hivi sasa zimeleta balaa na maafa.
Umoja wa mataifa wakati huo huo umeonya kuhusu uwezekano wa hali ya hatari ya magonjwa kusini mwa bara la Asia kutokana na mafuriko makubwa kabisa katika wiki za hivi karibuni ambapo watu kiasi 30 milioni nchini India, Bagladesh na Nepal wakiwa wanahitaji msaada mkubwa wa maji safi , chakula na nyumba.
Shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF pamoja na shirika la afya duniani WHO yana wasiwasi juu ya kusambaa kwa magonjwa yanayosababishwa na maji , homa na magonjwa ya ngozi, na yanatoa madawa ya dharura pamoja na vifaa vingine katika maeneo ambayo yameathirika.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva , Veronique Taveau wa shirika hilo ameonya kuwa mahitaji hayo yatakuwa kwa muda mrefu na kwamba watu wengi watabaki bila makaazi kwa muda wa wiki kadha.
Nao maafisa wa umoja wa Ulaya leo Alhamis wameahidi kutoa msaada kwa wahanga wa mafuriko katika eneo la kusini mwa bara la Asia , wakieleza masikitiko yao kuwa maafa hayo yanaweza kuwa mabaya zaidi.
Kamishna wa uhusiano na mataifa ya nje wa umoja wa Ulaya Benita Ferrero-Waldner amesema kuwa anasikitishwa mno na upotevu wa maisha ya watu kutokana na mafuriko haya kwa watu wengi katika eneo la Asia ya kusini.