Mafuriko yaathiri miji kadha nchini Australia
3 Januari 2011Jeshi la Australia leo limepeleka chakula na mahitaji mengine kwa watu walioathirika na mafuriko katika mji wa kaskazini wa Rockhampton kabla haujatengwa kabisa na sehemu nyingine za nchi hiyo , kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha maji katika janga la mafuriko ambapo watu kumi wamefariki.
Watu wapatao 200,000 wanakadiriwa kuwa wameathirika na mafuriko makubwa ambayo yamefunika karibu miji midogo 22 katika eneo la kaskazini la Australia, katika eneo ambalo ni sawa na ukubwa wa nchi za Ujermani na Ufaransa. Jeshi limekuwa likipeleka chakula na madawa katika mji wa Rockhampton , wenye wakaazi wapatao 75,000, wakati mji huo ulioko katika eneo la pwani ukijiweka tayari kwa mafuriko ambayo yanatarajiwa kuyatenga maeneo kadha na sehemu nyingine za mji huo.
Mji wa Rockhampton unaonekana kama uko katikati ya bahari, waziri mkuu wa jimbo la Qeensland, Anna Bligh, amesema baada ya kuangalia maafa hayo akiwa katika ndege. Kiasi cha maji kinachoelekea katika mji huo katika mito inayopitia karibu na mji huo kinashangaza.
Uwanja wa ndege umefungwa wakati mafuriko yamezuwia mawasiliano ya barabara upande wa kusini na magharibi, na kusababisha wasi wasi miongoni mwa maafisa kuwa eneo hilo lenye watu wengi huenda likapungukiwa na chakula.
Waziri mkuu Julia Gillard ametoa fedha za dharura kwa maeneo yaliyoathirika na mafuriko, ikiwa ni pamoja na wakulima ambao wamekuwa wakikabiliwa kwa muda mrefu na ukame, pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo.
Wakati mafuriko yatakapomalizika , tutaona madhara makubwa zaidi, lakini tutakuwa tunashirikiana na serikali ya jimbo hilo, kujenga upya miundo mbinu ya kijamii, Gillard amewaambia waandishi habari mjini Sydney.
Waziri mkuu Gillard ambaye alikagua maeneo ambayo yameathirika zaidi siku ya Ijumaa, amesema kuwa katika baadhi ya maeneo haya yamekuwa mafuriko makubwa kabisa ambayo hayajawahi kuonekana, na kutoa tahadhari kwamba kuna hatari zaidi kutokana na maji yanayokwenda kwa kasi. Mkurugenzi wa shirika la msalaba mwekundi katika jimbo la Queensland, Greg Goebel, amesema shirika lake limejiandaa kwa hali hiyo.
"Tuna nafasi ya watu 1,200, lakini hatutarajii kuwa idadi itakuwa juu sana, lakini tusisahau kuwa maji bado hayajafikia kiwango cha juu kabisa. Maji katika mji huu yanapanda kuelekea katika vituo vya uokozi tulivyoviweka na maji yanaelekea pia katika maeneo mengine , kwa hiyo watu wengi zaidi watakuja katika maeneo ya uokozi.
"Polisi wamethibitisha kufariki kwa mtu wa tatu tangu mafuriko hayo kutangazwa kuwa ni maafa, ambapo mtu mmoja alifariki baada ya gari lake kuchukuliwa na maji katika mto uliofurika. Watu kumi wamefariki hadi sasa tangu Novemba 30, ikiwa ni pamoja na magari matatu ambayo yamechukuliwa na maji.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Othman Miraj