Maendeleo ya haraka nini kimebadilika kupitia upigaji picha nchini Ujerumani
22 Septemba 2010Kuanzia jana tarehe 21 hadi tarehe 26 mwezi huu wa Septemba mjini Koln kunafanyika maonesho yanayojulikana kama "Photokina", ikiwa ni maonesho makubwa kabisa duniani ya vifaa vya kupigia picha pamoja na picha zenyewe.Karibu kamera milioni nane na nusu zilinunuliwa nchini Ujerumani mwaka uliopita. Maendeleo ya upigaji picha kwa kutumia kamera za digitali pamoja na uchukuaji picha za video umekuwa wa kasi sana , na sekta hii haina matatizo na teknolojia hii mpya. Ripoti ya Wolfgang Dick kuhusu nguvu ya picha, inasomwa humu studioni na Sekione Kitojo.
Ni uwezo gani, ambao simu za mkononi na kamera za digitali, pamoja na kamera ndogo za video zinaweza kufikia, kwa kweli zinakaribiana. Katika miaka ya 50 nchini Ujerumani kwa sekunde moja watu walikuwa wakibonyeza kitufe cha kupiga picha mara 100. Lakini hii leo kwa sekunde moja wanabonyeza watu mara 1,000. Constance Clauß kutoka umoja wa wenye viwanda vya kamera anazungumzia kuhusu mabadiliko katika jamii.
"Kamera iko katika nafasi ya tano, ambapo chombo hicho kinakuwa baada ya jokofu, televisheni, simu , pamoja na simu ya mkononi. Na kisha inakuja kamera".
Maendeleo ya teknolojia yanaelekea kila wakati kuleta chombo kidogo zaidi, kama kamera na uchukuaji picha za video katika simu ya mkononi, ambapo katika utafiti uliofanywa na wakfu wa Bertelsmann yameleta mabadiliko ya kidemokrasia katika jamii, na hali hii inaanzia katika familia , kama anavyoeleza Constanze Clauß.
"Hapo kabla alikuwapo mtu mmoja mkuu wa familia ambaye alikuwa akikamata kamera wakati wote. Hii leo kila mtu katika familia anataka kuwa na kamera yake. Anataka kufanya kumbukumbu yake, picha zenye mtazamo wake".
Upigaji picha wa digitali, ni wa kasi, rahisi, na unapatikana kila mahali. Swali ni iwapo katika hali halisi ni bora kuandika barua , barua pepe ama kutuma picha, asilimia 78 ya walioulizwa kati ya vijana wa miaka 15 hadi 30 wamejibu, wangependelea kutuma picha.
"Picha zina nguvu kubwa na kwa picha naweza haraka sana kusambaza habari".
Hata hapa Ujerumani kuna mitandao mingi ya kijamii, ambayo inafanyakazi kwa kutumia picha, ikiwa ni nguvu kuu ya mahusiano. Bila picha mitandao hiyo isingekuwapo tena.
Nafikiri ndio hali ilivyo. Wanaishi kwa ajili ya picha.
Picha ama picha za video ni kitu cha kawaida, kwa kuwa ni rahisi kuvibeba kwa kuwa ni ndogo. Hali hiyo inatumiwa kwa miaka minne hivi sasa na magezeti makubwa yenye wasomaji wengi hapa Ujerumani. Wanawaomba wasomaji wao kuwapatia picha muhimu za watu mashuhuri ama matukio ya muhimu. Michael Paustian ambaye ni kaimu mhariri mkuu wa gazeti la Bild Zeitung akizungumzia picha zinazotumwa na wasomaji wa gazeti hilo , amesema kuwa , hawa ni watu muhimu sana na wameleta mafanikio makubwa. Amesema kuwa gazeti linapata picha karibu 4,000 kwa siku. Katika miezi kumi na mbili iliyopita gazeti hilo limeweza kutengeneza karibu kurasa 1,000 za picha kutoka kwa wasomaji wa gazeti hilo.
Mwandishi : Dick , Wolfgang / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman.