Maelfu ya wakulima na matrekta yao kuandamana mjini Berlin
15 Januari 2024Kutwa nzima ya jana Jumapili, wakulima kutoka kila pembe ya Ujerumani walikuwa wanaelekea mjini Berlin ambako inaaminika zaidi ya matrekta 3,000 na malori 2,000 yataingizwa katikati ya mji.
Maandamano ya leo yanapangwa kufanyika mbele ya lango mashuhuri la Brandenburg na watu wapatao 10,000 wengi wakiwa ni wakulima wanatarajiwa kuhudhuria.
Maandamano hayo yaliyoanza Jumatatu iliyopita yameongeza shinikizo kwa serikali ya mseto ya Kansela Olaf Sholz ambayo bado inahangaika kutatua mzozo kuhusu bajeti ya mwaka ujao.
Shinikizo la wakulima limeilazimisha serikali kufutilia mbali mipango ya kuondoa nafuu ya kodi kwenye vyombo vya moto vinavyotumika kwa kilimo pamoja na kupendekeza kuondoa kwa awamu ruzuku inayotolewa na serikali kwenye mafuta ya Dizeli yanayoendesha mitambo mashambani.