1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji 1,500 wa Calais wajaribu kuingia Uingereza

29 Julai 2015

Kiasi ya wahamiaji 1,500 wanaojaribu kuingia Uingereza wamefanya jaribio jingine la kuingia nchini humo kupitia njia inayosafirisha malori ya mizigo kutoka mji wa bandarini wa Calais nchini Ufaransa.

https://p.dw.com/p/1G6kX
Picha: Denis Charlet/AFP/Getty Images

Jaribio hilo la hivi punde linakuja baada ya wahamiaji 2,000 kujaribu hapo jana kuingia Uingereza kupitia njia hiyo ya mpakani katika mji wa bandarini wa Calais bila ya mafanikio.

Msemaji wa kampuni ya usafiri ya Eurotunnel amesema hii leo wafanyakazi wa kampuni hiyo wamepata mwili wa mhamiaji anayeaminika kuwa raia wa Sudan aliye kati ya umri wa miaka 25 na 30 aliyegongwa na lori.

Idadi ya wahamiaji ambao wamefariki wakijaribu kuingia Uingereza kupitia kivuko hicho tangu mwezi uliopita imefikia watu tisa. Usalama umeimarishwa katika bandari ya Calais tangu kati kati ya mwezi uliopita ili kuwazuia wahamiaji kuingia Uingereza na sasa wameamua kutumia mbinu hata hatari zaidi za usafiri kujaribu kuingia nchini humo.

Uingereza yatiwa wasiwasi na wahamiaji

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ameelezea wasiwasi kuhusu matukio hayo ya hivi punde ya maelfu ya wahamiaji kujaribu kuingia nchini mwake wakitokea mji wa Ufaransa wa Calais.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron
Waziri mkuu wa Uingereza David CameronPicha: picture alliance/empics/P. Ellis

Cameron ambaye yuko ziarani Singapore amesema hali hiyo inatia wasiwasi na kuongeza kuwa wanashirikiana kwa karibu na maafisa wa Ufaransa kushughulikia tatizo hilo.

Waziri huyo mkuu wa Uingereza amesema watafanya kila njia kuepusha visa vya wahamiaji kuingia Uingereza kwa njia zisizo halali na wanazingatia uwezekano wa kuzungusha senyenge katika eneo hilo la mpakani.

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Theresa May anatarajiwa kufanya mkutano na kamati ya serikali ya kushughulikia masuala ya dharura kuijadili hali hiyo.

May amesema serikali yake itatumia kiasi cha paundi milioni saba kuisaidia Ufaransa kuimarisha usalama katika kivukio hicho. Tayari Uingereza imetumia euro milioni 4.7 kuweka vizuizi kuimarisha shughuli za kushika doria katika eneo hilo.

Ufaransa na Uingereza kushirikiana zaidi

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Bernard Cazeneuve alikuwa ziarani mjini London hapo jana kufanya mazungumzo na May kuhusu namna za kukabiliana na tatizo hilo la wahamiaji ambalo limekuwa suala msumari moto kati ya nchi hizo mbili kwa miaka. Cazeneuve amesema wahamiaji kadhaa waliojaribu kuingia Uingereza wamekamatwa na hali imedhibitiwa Calais.

Baadhi ya wahamiaji wakitegea usafiri katika bandari ya Calais
Baadhi ya wahamiaji wakitegea usafiri katika bandari ya CalaisPicha: Reuters/V. Kessler

Kampuni ya eurotunnel inatafuta fidia ya euro milioni 9.7 kutoka kwa serikali za Ufaransa na Uingereza kutokana na hasara iliyopata kutokana na kusitishwa na kucheleweshwa kwa huduma zake za usafiri,hali iliosbabibishwa na vurumai hiyo ya wakimbizi katika kipindi cha siku mbili zilizopita.

Kwa wiki kadhaa, kumekuwa na majaribio chungu nzima ya wahamiaji hao kujaribu kutumia njia za chini kwa chini za usafiri wa reli, feri na malori zinazosimamiwa na kampuni ya eurotunnel huku idadi hiyo ya wahamiaji ikizidi kupanda kila uchao katika siku za hivi karibuni.

Kulingana na takwimu rasmi iliyotolewa mapema mwezi huu kuna kiasi ya wahamiaji 3,000 katika mji huo wa bandarini waliokita kambi wakisubiri kuvuka kwa kila namna kuingia Uingereza. Wengi wa wahamiaji hao wanatokea Ethiopia, Eritrea, Sudan na Afghanistan.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Hamidou Oummilkheir