Maelfu ya wafanyakazi wa umma waandamana Ubelgiji
16 Desemba 2022Maelfu ya wafanyakazi wa sekta ya umma nchini Ubelgiji wameandamana leo kwenye viunga vya mji mkuu Brussels, kuitaka serikali kuongeza viwango vya mishahara na kuchukua hatua zaidi kuwasaidia kuhimili gharama kubwa za nishati.
Licha ya hali ya hewa ya baridi kali, zaidi ya wafanyakazi 16,000 walitembea kuzunguka mji huo mkuu kuishinikiza serikali kuongeza malipo ya mishahara na marupurupu katika wakati mfumuko wa bei umevunja rikodi kwenye mataifa mengi ya Ulaya.
Pamoja na mambo mengine waandamanaji hao chini ya mwavuli wa vyama vitatu vikubwa vya wafanyakazi, wanaitaka serikali kuweka ukomo wa bei za nishati na kupunguza viwango vya kodi.
Maandamano hayo ya leo yalitatiza shughuli za usafiri mjini Brussels ikiwemo njia za reli na katika uwanja wa ndege wa mji huo.