1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya wachungaji watoroka kusini mwa Nigeria

12 Februari 2021

Takriban wafugaji elfu 4 wa kabila la Fulani wametoroka Kusini mwa Nigeria katika muda wa wiki moja iliyopita kufuatia mashambulizi kutoka kwa magenge ya watu yanaowalaumu kwa ongezeko la uhalifu katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/3pGUI
Niger Normaden Fulani Scharfherde bei Gadabeji
Picha: AP

 

Katika wiki za hivi karibuni, kumekuwa na mashambulizi dhidi ya makazi ya wafugaji wa kabila la Fulani linalozungumza lugha ya Kiyoruba katika eneo la Kusini Magharibi mwa Nigeria na wale wanaozungumza lugha ya Igbo katika eneo la Kusini Mashariki kutoka kwa magenga ya jamii za eneo hilo.

Wafugaji hao wanashtumiwa kwa kuchangia katika visa vya utekaji nyara pamoja na mapigano ya ghasia kati yao na wakulima kuhusiana na haki ya kulisha mifugo hali inayochochea zaidi mvutano wa kijamii katika taifa hilo la watu milioni 200 lililo na makabila mengi. Mkuu wa shirika la usimamizi wa masuala ya dharura (SEMA) katika jimbo la Kaskazini la Kaduna Hussaini Abdullahi, ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba wafugaji wengi bado wanawasili katika eneo hilo na kwamba serikali itawasaidia kujipanga kimaisha. Abdullahi ameongeza kuwa mahitaji yao makubwa ni chakula na bidhaa za nyumbani kwa sababu hawakuja na kitu na wamepoteza kila kitu.

Eneo walilopewa makazi

A young fulani herdsmen
Mchungaji wa kabila la Fulani nchini NigeriaPicha: DW

Mkuu wa shirika la wafugaji wa kabila la Fulani (MACBAN) katika jimbo hilo Haruna Usman Dugga, amesema wafugaji hao wamepewa makazi katika mbuga ya wanyama. Dugga ameongeza kuwa wafugaji hao elfu 4 wa kabila la Fulani wanaozijumuisha familia 150, wamehamia katika mbuga ya wanyama ya Labduga katika muda wa wiki moja iliyopita na kwamba wengine bado wako njiani kuelekea katika eneo hilo. Dugga amesema, ijapokuwa kumekuwa na wito wa kurejea kwa wafugaji wote wa kabila la Fulani walioko katika eneo hilo la Kusini, haijakuwa rahisi kwa wao kufanya hivyo na kuongeza kwamba wafugaji hao katika eneo la Kusini wamekuwa katika eneo hilo kwa miaka mingi hivyo kufanya kuwa vigumu kuwataka waondoke.

Dugga ameongeza kusema kuwa malisho ya mifugo yao ni suala lingine litakalowafanya baadhi kupendelea kubaki katika eneo hilo kwa sababu hakuna mimea ya kutosha katika eneo la Kaskazini.

Hofu ya mashambulizi ya kulipiza kisasi

Siku ya Jumanne, magavana kutoka eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo walitahadharisha kuhusu mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya watu kutoka eneo la Kusini walioko katika eneo hilo. Walitoa wito kwa viongozi wa eneo la Kusini kusitisha mashambulizi dhidi ya wafugaji wa kabila la Fulani kuzuia kuitumbukiza Nigeria katika mizozo ya kijamii.

Wachambuzi pia wameonya dhidi ya kuchanganya matatizo ya usalama wa kitaifa hasa miaka ya mapigano makali kati ya wafugaji na wakulima kuwania maji na haki za kulisha mifugo. Rais Muhammadu Buhari tayari yuko chini ya shinikizo kali la kukabiliana na uasi wa muongo mmoja wa makundi ya  itikadi kali katika eneo la Kaskazini Mashariki na kuongezeka kwa ghasia za magenge ya uhalifu katika eneo la Kaskazini Magharibi. Mchambuzi mmoja katika eneo hilo Ibrahim Adamu, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mvutano huo wa kijamii utaongeza ghasia kati ya wafugaji na wakulima zinazoshuhudiwa kote katika eneo la Kaskazini na kwamba serikali inapaswa kutafuta sulushisho la tatizo hilo.