1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wamuaga George Floyd kabla ya mazishi yake

9 Juni 2020

George Floyd, Mmarekani mweusi mwenye umri wa miaka 46 ambaye mauaji yake na polisi mweupe yamembadilisha kuwa picha ya ulimwengu ya mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi, atazikwa leo mjini Houston

https://p.dw.com/p/3dTrJ
USA Houston | Hunderte nahmen Abschied von George Floyd
Picha: Reuters/G. A. Vasquez

George Floyd, Mmarekani mweusi mwenye umri wa miaka 46 ambaye mauaji yake na polisi mweupe yamembadilisha kuwa picha ya ulimwengu ya mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi, atazikwa leo mjini Houston, ambako alikulia.

Waombolezaji wengi walitengeneza ishara ya msalaba wakati wakikaribia jeneza la Floyd lililokuwa wazi, katika kanisa la The Fountain of Praise mjini Houston, jimbo la Texas, kutoa heshima zao za mwisho wakati wengine wakipiga magoti au kuinamisha vichwa na kumuombea kimyakimya mtu ambaye amekuwa ishara ya karibuni ya vuguvugu la kupinga ubaguzi wa rangi Marekani.

Hafla hiyo ilikuwa ya mwisho katika msururu wa hafla zilizoandaliwa za kumuaga Floyd. Atazikwa leo katika mazishi ya faragha kando ya kaburi la mamake mjini Houston, ambako ndiko alikokulia.

Mjini Washington, wajumbe wa Democratic walipiga magoti na kusalia kimya kwa dakika nane na sekunde 46, muda alioutumia polisi mweupe kugandamiza shingo ya Floyd akitumia goti.

Wademocrat wamewasilisha mswada wa sheria za kuimarisha udhibiti wa polisi, ikiwa ni mojawapo ya masharti muhimu ambayo waandamanaji wanadai. Marekani imeshuhudia maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa ya kudai haki tangu mauaji ya Maetin Luther King Jr.

Miongoni mwa mambo yaliyomo kwenye muswada huo ni kupigwa marufuku mshukiwa kugandamizwa shingo, kurahisisha malalamiko dhidi ya polisi na kuwezesha uchunguzi huru. Nancy Pelosi ni spika wa Bunge

Hatua hiyo ya Baraza la Wawakilishi inakuja siku moja baada ya halmashauri ya mji wa Minneapolis kupiga kura ya kuvunja na kujenga upya idera ya polisi mjini humo ambako Floyd alifariki wakati akikamatwa mnamo Mei 25.

Derek Chauvin, polisi mweupe aliyeonekana kwenye video akigandamiza shingo ya Floyd kwa kutumia goti wakati akiwa amefungwa pingu, kwa karibu dakika tisa, alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.

Jaji anayeendesha kesi hiyo alimuwekewa dhamana ya dola milioni moja. Chauvin mwenye umri wa miaka 44, aliunganishwa na kikao cha mahakama kwa njia ya video akiwa gerezani. Jaji alitangaza masharti kadhaa ya kuwachiwa kwake kwa dhamana. Mshukiwa huyo hapaswi kuondoka jimbo la Minnesota baada ya kuwachiwa, asiwasiliane na familia ya Floyd na lazima asalimishe silaha zote anazomiliki. Aidha haruhusiwi kufanya kazi katika nafasi yoyote kwenye idara ya usalama. Polisi wengine watatu wa Minneapolis walifikishwa mahakamani wiki iliyopita wakikabiliwa na mashitaka ya kusaidia katika mauaji ya Floyd. Wote wanne wamefutwa kazi.

Mgombea wa urais wa chama cha Democratic Joe Biden, alikwenda Houston kukutana na wanafamilia ya Floyd. Tayari baadhi ya miji ya Marekani imeanza kufanya mageuzi  - kwa kuanza na marufuku ya matumizi ya mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira.