1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakusanyika Nairobi kumuapisha Odinga

30 Januari 2018

Zaidi ya wafuasi 2,000 wa kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga wamekusanyika siku ya Jumanne katika bustani mjini Nairobi ambako alitarajiwa kula kiapo cha urais, katika hatua ya kumpinga rais Uhuru Kenyatta.

https://p.dw.com/p/2rkTf
Kenia Vereidigung von Raila Odinga in Uhuru Park in Nairobi
Wafuasi wa NASA wakisubiri kuapishwa kwa kiongozi wao Raila Odinga katika bustani ya uhuru mjini Nairobi, Jumanne 30.01.2018Picha: DW/S. Wassilwa

Kenyatta aliapishwa kwa muhula wa pili mwezi Novemba baada ya kushinda uchaguzi wa marudio ambao Odinga aliususia, kutokana na mashaka ya kutokuwa huru na wa haki. Awali, mwanasheria mkuu wa Kenya alionya kuwa Odinga angekabiliwa na mashitaka ya uhaini iwapo tukio hafla hiyo ingeendelea kufanyika. Adhabu ya kosa la uhaini ni kifo.

Vituo kadhaa vya redio na televisheni vimezimwa Jumanne asubuhi kuzuwia urushaji wowote wa moja kwa moja wa tukio hilo, linalofanyika katika Bustani ya Uhuru mjini Nairobi.

"Maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya kumuapisha rais na naibu rais wa Jamhuri ya Kenya. Uhuru unakuja," Muungano wa Odinga wa NASA uliandika kwenye ukurasa wake wa twitter mapema Jumanne, ukionyesha picha za video za eneo la tukio.

Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa maelfu walikuwa wanakusanyika katika bustani ya uhuru. Kufikia saa mbili asubuhi, zaidi ya watu 2,000 walikuwa wamewasili katika bustani hiyo, iliyoko karibu na wilaya kuu ya bishara mjini Nairobi. wengi walikuwa wakiimba nyimbo za kumsifu Odinga huku wakipeperusha matawi ya miti.

Raila Odinga
Raila Odinga anadai yeye ndiyo mshindi halali wa uchaguzi wa rais nchini Kenya.Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

"Ondinga ndiye tunamtambua kama rais na hiyo ndiyo sababu tunamuapisha," alisema kinyozi Benta Akinyi mwenye umri wa miaka 32, akiwa amesimama karibu na wafuasi wengine wa upinzani wanaopuliza tarumbeta na firimbi.

 

Vyombo vya usalama vyatoweka

Ingawa polisi ilikuwa imesema ingezuwia mikusanyiko yoyote inayofanyika kinyume na sheria siku ya Jumanne, hakukuwa na askari wowote waliovalia sare katika bustani hiyo, na wala hakukuwepo na maafisa wa kuzuwia ghasia au magari ya polisi.

Karibu watu 100 waliuawa katika vurugu zinazohusiana na uchaguzi huo, wengi wao katika makabiliano kati ya wafuasi wa Odinga na jeshi la polisi. Kituo cha redio cha Capital FM, kuwa wafuasi wa Odinga walipewa idhini na mamla za Kenya kutumia bustani hiyo.

Wasemaji wa polisi na serikali hawakupatikana kuzungumzia ripoti hizo. "Tunataka kulifanya tukio letu kwa amani," muungano wa Odinga ulisema katikataarifa Jumatatu jioni.

"Pamoja na hayo tunapenda kuitahadharisha serikali ya Jubilee kwamba tutatimiza lengo letu kwa namna yoyote ile. Tunawashauri wafuasi wetu waje wakiwa wamejindaa kubakia hadi lengo litimie."

Kenia Vereidigung von Raila Odinga in Uhuru Park in Nairobi
Wafuasi wa muungano wa NASA wakiwa katika bustani ya Uhuru mjini Nairobi wakisubiri kuapishwa kwa Raila Odinga, Jumanne 30.01.2018.Picha: DW/S. Wassilwa

Vituo vya utangazi vyazimwa

Kufikia saa moja na dakika 20 asubuhi, vituo kadhaa vya utanganzaji, vikiwemo redio na televisheni ya Citizen, televisheni za NTV na KTN, zilizokuw azinatangaza moja kwa moja kutokea bustani ya Uhuru, zilisema zilikuwa zimezimwa na mamlaka za serikali.

Msemaji wa mamlaka ya mawasiliano ya Kenya alisema walikuwa kwenye mkutano na kwamba angetoa tamko baadae. "Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya imezima mitambo ya televisheni ya Citizen na redio katika maeneo mengi ya nchi kuhusiana na urushaji mubashara wa mipango ya uapishwaji ya NASA," Citizen ilisema kwenye mtandao wake wa intaneti.

Siku ya Jumatatu, mwenyekiti wa jukwaa la wahariri nchini Kenya, Linus Kaikai, alisema wahariri wandamizi waliitwa na mamlaka kuonywa dhidi ya kuripoti tukio hiyo, vinginevyo wakabiliwe na hatari ya kufungiwa.

Mwandishi. Iddi Ssessanga/rtre, dpae

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman