1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakusanyika kumkumbuka Hariri, Lebanon

Charles Mwebeya14 Februari 2007

Makumi ya maelfu ya walebanon wakipeperusha bendera na kurusha hewani maputo yenye rangi ya bluu, wamekusanyika mjini Beirut kukumbuka mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafik Hariri.

https://p.dw.com/p/CHKA

Kumekuwapo na ulinzi mkali katika kaburi la Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Syria katika eneo la mashujaa ambapo zinaonekana namba 730, zikiashiria siku 730 kupita toka kuuawa kwake ilhali muuaji akiwa bado hajapatikana.

Wafuasi hao ambao wengi ni wale wanaoiunga mkono Serikali na kuishutumu Syria kuhusika na kifo cha kiongozi huyo miaka miwili iliyopita, wamekusanyika kwa wingi katika eneo la mashujaa huku wakitenganishwa na uzio maalum na wale wa upinzani.

Wafuasi wa upande wa serikali wanaishutumu Syria kuhusika na kifo cha waziri mkuu wa huyo wa zamani wa Lebanon February 14 , mwaka 2005,kutokana na shambulio la bomu.

Hata hivyo Syria ilikanusha kuhusika katika mauaji hayo hatua iliyopelekea jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kuitaka Syria kuondoa majeshi yake yaliyokaa nchini Lebanon kwa takribani miaka 29.

Waziri Mkuu wa Lebanon Fuad Siniora ameifanya siku ya February 14 kila mwaka , kuwa siku ya kitaifa ya kumbukumbu ya Waziri mkuu huyo wa zamani Rafik Hariri, ambapo maduka, shule na biashara hufungwa.

Mtoto wa kiume wa Marehemu Hariri, Saad ambaye anaongoza harakati dhidi ya kundi la Hezbollah, ametoa wito wa kuiunga mkono serikali .

Mkusanyiko na maandamano hayo unakuja siku tatu baada ya mlipuko wa bomu kusababisha vifo vya watu watatu mjini Beirut.

Serikali ya muungano ikiongozwa na waziri mkuu Fuad Siniora tayari imeishutumu Syria kuhusika na shambulio hilo la juzi.

Hata hivyo katika maandamano ya leo ulinzi mkali umeimarishwa katika mitaa yote mjini Beirut, na mpaka hivi sasa hakujaripotiwa ghasia zozote kuhusiana na maandamano hayo.

Lebanon imekuwa katika mvutano mkubwa wa ndani kwa ndani, baina ya wafuasi wa serikali ambao wengi wao ni kutoka madhehebu ya Sunni, na wale wa upinzani wa madhehebu ya shia , ambao wanaliunga mkono kundi la Hizbollah na Amal , makundi yanayosadikiwa kufadhiliwa na Syria.

Hali ya wasiwasi nchini Lebanon ilianza toka mwezi November mwaka jana, baada ya mawaziri sita wanaoungwa mkono na serikali ya Syria wakilazimika kujiuzulu baada ya kuhusishwa na kifo cha Bwana Hariri na tume maalum ya uchunguzi ya umoja wa mataifa.

Wiki iliyopita Umoja wa mataifa ulitia saini makubaliano ambayo yalilenga kuwafikisha katika mahakama ya kimataifa maafisa wa ngazi za juu wa Syria na Lebanon wanaohusishwa na kifo hicho.

Makundi ya Hezbollah na Amal yamesema yanaunga mkono wazo la Mahakama ya kimataifa ila wanataka majadiliano zaidi juu ya mamlaka ya mahakama hiyo.