Maelfu waihama Somalia sababu ya ukame
10 Februari 2017Serikali za mikoa na maafisa wa shirika la kuwasaidia watoto la Save the Children wanaripoti kwamba mamia ya malori yaliyosheheni familia na mifugo yamekuwa yakiwasili katika maeneo ya pwani ya Puntland katika kipindi cha wiki sita zilizopita na yamekuwa yakiwapeleka katika maeneo ya mbali kama Somaliland, kwa kuwa walisikia kwamba kulinyesha mvua kabla sikukuu ya Krismasi mwaka uliopita.
Katika eneo la kati upande wa kusini mwa Somalia, Umoja wa Mataifa unaripoti kwamba zaidi ya wakimbizi 100 wasomali waliokabiliwa na ukame wamekuwa wakivuka mpaka wa Ethiopia na kuingia kambi ya Dollo Ado tangu mwezi Januari, jambo ambalo halijaonekana katika miaka minne.
Watu milioni 6 wakabiliwa na uhaba wa chakula
Huko Puntland, eneo linalokabiliwa na ukame mbaya zaidi tangu mwaka wa 1950, wakimbizi wapya wa ndani waliopoteza mifugo wao wanakusanyika katika kambi zisizo rasmi wakitafuta maji, chakula na misaada. Ingawa familia zinapata wakati mgumu kukabiliana na hali hiyo kutokana na bei za juu za maji na chakula.
"Hali ya ukame imekuwa mbaya na haijawahi kuwa hivi kwa miongo kadhaa na mizoga ya mbuzi imezagaa kila mahali," alisema kwenye taarifa Hassan Noor Saadi mkurugenzi wa shirika la Save the Children nchini Somalia.
Kutokana na hali hiyo Umoja wa Mataifa ulitoa tahadhari ya kutokea kiangazi kwa Somalia mapema mwezi huu, ukisema zaidi ya watu milioni 6 wanakabiliwa na tatizo la usalama wa upatikanaji wa chakula.
Ukame umetokana na uhaba wa mvua
Watoto 71,000 tayari wanakumbwa na utapia mlo na wako katika hatari ya kuaga dunia, huku zaidi ya watoto 360,000 walio chini ya miaka 5 wakikabiliwa na tatizo hilo kulingana na shirika la Save the Children.
Kwa mujibu wa wa Umoja wa Mataifa, Somalia imeshuhudia misimu ya kufuatana ya uhaba wa mvua, hii ikiwa na maana kwamba ukame tayari umeharibu mimea na kuuwa mifugo katika maeneo yaliyoathirika zaidi. Ukame huu wa sasa umeyaathiri mataifa jirani ya Kenya na Ethiopia.
Huku watabiri wa hali ya hewa wakibashiri mvua haba katika miezi kadhaa ijayo nchini Somalia, nchi hiyo itajikuta katika hali mbaya zaidi ya ukame iwapo hakutatolewa fedha za misaada, maji na dawa ili ziwafikie wale walioathirika zaidi hususan watoto.
Ukame nchini Somalia kati ya mwaka 2010 na 2012 ulikadiriwa kuwauwa watu kati ya 260,000, wengi wao watoto.
Mwandishi: Jacob Safari/DPA/Save The Children
Mhariri: Josephat Charo