1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana kupinga sheria yenye utata Georgia

15 Mei 2024

Makundi makubwaya waandamanaji yalifurika kwenye mitaa ya mji mkuu wa Georgia usiku wa kuamkia leo baada ya wabunge kuidhinisha sheria tata.

https://p.dw.com/p/4fs6A
Maandamano mjini Tbilisi
Waandamanaji wakiwa wamefurika kwenye mitaa ya mji mkuu wa Georgia Picha: Mikhail Yegikov/Tass/dpa/picture alliance

Makundi makubwa ya waandamanaji yalifurika kwenye mitaa ya mji mkuu wa Georgia usiku wa kuamkia leo baada ya wabunge kuidhinisha sheria tata ambayo wakosoaji wanasema inatishia uhuru wa kujieleza na kuyaweka rehani matarajio ya nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Baada ya kupitishwa sheria hiyo ambayo serikali mjini Tblisi inasema inalenga kuzuia "ushawishi wa kigeni" nchini Georgia, waandamanaji waliokusanyika nje ya majengo ya bunge walijaribu kuvunja vizuizi vya chuma huku wakipiga mayowe kwa hasira.

Maandamano yaliendelea usiku kucha kwa maelfu ya kukusanyika kwenye viwanja vya mashujaa katikati mwa mji mkuu,  Tbilisi.

Sheria hiyo ambayo wale wanaoipinga wanasema imechukua mtindo wa kirusi, inavitaka vyombo vya habari na mashirika ya kiraia kujiandikisha kama "walinda maslahi ya kigeni" iwapo wanapokea zaidi ya asilimia 20 ya fedha kutoka nje.

Umoja wa Ulaya na Marekani zimeionya serikali ya Georgia kuhusu sheria hiyo, huku kila upande ukisema unatiwa mashaka na dhamira ya kutungwa sheria hiyo.