Maelfu waandamana Hungary kuhusu kashfa ya unyanyasaji
17 Februari 2024Matangazo
Maelfu ya watu waliandamana jana katika mji mkuu wa Hungary wa Budapest kupinga msamaha wa rais katika kesi ya unyanyasaji kingono watoto ambayo imekuwa mwiba wa kisiasa kwa waziri mkuu Viktor Orban. Orban hajazungumzia kashfa hiyo, lakini anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kila mwaka ya hali ya taifa siku ya Jumamosi.
Mnamo Jumamosi iliyopita, rais wa Hungary na waziri wa zamani wa sheria Judit Varga, walijiuzulu baada ya kuunga mkono uamuzi wa kutoa msamaha kwa mwanamume aliyehusishwa na kashfa ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto mwaka 2023.
Kiongozi mwingine mkubwa wa kanisa la Kiprotestanti Askofu Zoltan Balog alitangaza kujiuzulu jana kuhusiana na kashfa hiyo. Askofu huyo aliwahi kuhudumu kama waziri wa serikali kipindi cha nyuma.