1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana duniani kuadhimisha Mei Mosi

1 Mei 2019

Leo ni Siku ya Wafanyakazi Duniani, ambapo wafanyakazi wa sekta za umma na za binafsi wanaiadhimisha siku hii kwa kuandamana huku ukitolewa ujumbe pamoja na salamu mbalimbali kuzitaka serikali kuimarisha hali zao.

https://p.dw.com/p/3HlCm
Russland - Demonstrationen zum 1. Mai
Picha: picture-alliance/dpa/TASS/K. Kukhmar

Kauli mbiu ya siku hii ambayo huadhimishwa kila Mei Mosi kwa mwaka huu 2019 ni ''Pensheni ya Kudumu kwa wote: Wajibu wa Washirika wa Kijamii''. Vyama vya wafanyakazi na kijamii vinaiadhimisha siku hii kwa kuandaa mipango mbalimbali itakayosaidia kuimarisha mishahara ya wafanyakazi pamoja na mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

Mandamano mbalimbali yanafanyika leo, ambapo katika bara la Asia wafanyakazi wanakusanyika kwenye miji mikuu ya nchi za Korea Kusini, Ufilipino, Malaysia, Indonesia, Taiwan, Cambodia na Myanmar wakidai mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Maelfu ya vyama vya wafanyakazi na wanaharakati wanataka kuzingatiwa na kuheshimiwa kwa haki za wafanyakazi kwa ujumla.

Kuimarishwa haki za wafanyakazi

Nchini Korea Kusini muungano wa vyama vya wafanyakazi umetoa taarifa ya pamoja na vyama vya wafanyakazi wa Korea Kaskazini wakizishinikiza nchi zao kuyatekeleza yale yaliyofikiwa katika mikutano kadhaa ya kilele kati ya Korea hizo mbili, mwaka uliopita. Msemaji wa Shirikisho la Wafanyakazi Korea Kusini Kim Hyong-Sok ametoa wito wa kuimarishwa kwa haki na mikataba ya wafanyakazi

''Waajiri wa Korea Kusini hawataki kuwapa wafanyakazi nguvu zaidi, badala yake wanalinda mamlaka yao na wamekuwa wakivishambulia vyama vya wafanyakazi. Tunachotaka sisi ni kuzingatiwa na kuimarishwa kwa haki za wafanyakazi wote,'' alisema Hyong-Sok.

Mingi ya miradi iliyokubaliwa katika mazungumzo hayo, ukiwemo ule wa kiuchumi, inakwamishwa na kutokuendelea kwa mchakato wa mazungumzo ya nyuklia kati ya Korea Kaskazini na Marekani.

Reiner Hoffmann DGB-Vorsitzender
Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Ujerumani, DGB, Reiner HoffmannPicha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Nchini Ujerumani, shirikisho la vyama vya wafanyakazi, DGB limewataka wafanyakazi kuandamana kudai kuwepo kima cha chini cha mshahara ambacho ni sawa kote barani Ulaya. Mwenyekiti wa DGB, Reiner Hoffmann amewataka wapiga kura kuhakikisha kura zao zinaleta maana katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya baadae mwezi huu.

Maandamano makubwa yanafanyika kwenye mji wa mashariki wa Leipzig, lakini wanachama wa vyama vya wafanyakazi wanakutana pia mjini Berlin katika lango maarufu na la kihistoria la Brandenburg.

Usalama waimarishwa Ufaransa

Aidha, Ufaransa kwa upande wake imeimarisha usalama katika maandamano ya Siku ya Wafanyakazi, huku wizara ya mambo ya ndani ikisema kuna hatari kwamba ''wanaharakati wenye msimamo mkali'' wanaweza kujiunga na maandamano ya kuipinga serikali ya vizibao vya njano pamoja na vyama vya wafanyakazi katika mitaa ya Paris na kwenye miji mingine ya nchi hiyo.

Vyama vya wafanyakazi na chama cha Kikomunisti pia wanaandamana nchini Urusi katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Maandamano ya vyama vya wafanyakazi na vile vya kisiasa yamefutwa nchiri Sri Lanka, kwa sababu ya hofu ya kiusalama kutokana na mashambulizi yaliyofanywa Jumapili ya Pasaka na kuwaua watu 253. Wanamgambo wenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS wamekiri kuhusika na mashambulizi hayo.