Maelfu waandamana dhidi ya chama cha AfD
25 Septemba 2017Chama cha AfD kitangia katika bunge la shirikisho Bundestag kwa mara ya kwanza katika historia yake kufuatia uchaguzi mkuu wa taifa uliofanyika siku ya Jumapili.
Kiasi ya waandamanaji 1,000 walijikusanya nje ya klabu ya usiku katika eneo la Alexanderpatz mjini Berlin ambako chama cha AfD kilikuwa kinafanya sherehe zake za kushangiria matokeo ya uchaguzi.
Waandamanaji walipiga makelele " Ondokeni , Ondokeni , na AfD , wabaguzi duni !"
Mamia kadhaa ya watu pia walijikusanya kwa ajili ya maandamano ya ghafla katika mji wa mashariki wa Leipzig, Maandamano mengine yaliripotiwa mjini Kolon, Hamburg na Frankfurt. Katika maandamano mjini Kolon , ambapo watu karibu 400 walishiriki , yalikuwa ni sehemu ya kampeni ya nchi nzima iliyopewa jina la "siasa za kizalendo sio mbadala."
Mtandaoni hashtag moja ilikuwa ni miongoni mwa mada tano zilizokuwa zikiwashughulisha sana watu waliongia katika mitandao ya jamii katika twitter nchini Ujeruimani kwa sehemu kubwa ya jioni.
Wale ambao hawakuunga mkono chama cha AfD , ambacho kimepata asilimia 13 ya kura , walitumia "hashtag 187percent" kusisitiza ukweli kwamba walipiga kura zao kwa vyama vikuu.
Mmoja wa waandamanaji Peter Palberg amesema:
"Hawa ni Wanazi tu. Ukiangalia wanasiasa wao na lugha wanayotumia. Inakumbusha kwa kiasi kikubwa enzi zilizopita."
Kwa wiki kadhaa , kansela Angela Merkel alilazimika kukabiliana na kuzomewa na miluzi kila mahali alikokwenda katika kampeni katika jimbo anakotoka mashariki mwa Ujerumani.
Wapiga kura wa mashariki
Na jana Jumapili, ilikuwa ni wapiga kura wa mashariki, waliokasirishwa na uamuzi wake wa kuwaruhusu wakimbizi mamia kwa maelfu kuingia nchini humo, ambapo kulipelekea kukipatia chama chake cha kihafidhina matokeo mabaya kabisa tangu mwaka 1949 na kusababisha chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kuingia bungeni.
Muandamanaji mmoja Jonas Ockelmann Berlin alisema.
"Binafsi nimeathirika na kuingia kwa chama cha AfD katika bunge. Siasa zao zinaniathiri. Wanapinga mashoga na wanawake. Hawataki vitabu vya kiada vinavyoonesha wanawake wenye mahusiano ya kimapenzi."
Matokeo hayo yanaashiria kwamba taasisi zinazokusanya maoni ya wapiga kura huenda walipuuzia athari za mzozo wa wakimbizi katika uchaguzi huu na ushawishi mkubwa ambao ungepatikana kutoka upande wa mashariki mwa Ujerumani, ambako wapiga kura wanaendelea kuwa na mwelekeo tofauti kabisa na wenzao wa upande wa magharibi miaka 28 baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin.
Wakati baraza kuu la Wayahudi nchini Ujerumani limesema ongezeko la uungwaji mkono kwa chama cha AfD ni changamoto kubwa inayoikabili Ujerumani baada ya vita vikuu vya dunia , kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ufaransa Marine Le Pen amekipongeza chama cha AfD kwa "matokeo yao ya kihistoria."
Nae rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amempongeza leo kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa ushindi wake, akiahidi kwamba washirika wawili hao wa Ulaya wataendeleza ushirikiano wao muhimu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Zainab Aziz