Maduro amshambulia mpinzani aliyejitangaza kuwa rais
25 Januari 2019Hatua hiyo inatazamiwa kuzusha mapambano makali ya madaraka katika taifa hilo la Amerika Kusini linalokumbwa na mgogoro. Maduro aliwaita nyumbani wanadiplomasia wote wa Venezuela waanofanya kazi Marekani na kufunga ubalozi wake jana, siku moja baada ya kuwaamuru wanadiplomasia wa Marekani kuondoka Venezuela ifikapo mwishoni mwa wiki hii kwa sababu Rais Donald Trump aliunga mkono hatua ya Juan Guiado kujiangaza kuwa rais "nimefanya uamuzi kwa kuzingatia sheria ya kitaifa, sheria ya kimataifa, kama kiongozi wa nchi na serikali, nimeamua kuvunja mahusiano ya kidiplomasia na kisiasa na serikali ya kibeberu ya Donald Trump na kuwafukuza wafanyakazi wake wote wa kidiplomasia kutoka Venezuela". Alisema Maduro
Marekani imekataa kutii amri hiyo, lakini imewaamuru wafanyakazi wake wasiokuwa na majukumu yenye umuhimu mkubwa kuondoka nchini humo, ikitaja wasiwasi wa usalama.
Utawala wa Trump unasema amri ya Maduro sio halali kwa sababu Marekani haimtambui tena kuwa kiongozi halali wa Venezuela.
Wakati huo huo, macho yote yapo kwa Guaido ambaye hajulikani aliko tangu kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 35 alipoapishwa kiishara siku ya Jumatano mbele ya maelfu ya wafuasi waliomshangilia, akiapa kuilinda katiba na kuiondoa Venezuela kutoka kwenye uongozi wa kiimla wa Maduro. Akizungumza kutoka eneo lisilojulikana, Guaido ameiambia televisheni ya Univision kuwa atazingatia kumpa msamaha Maduro na washirika wake kama watasaidia kuirejesha Venezuela katika hali ya demokrasia.
Viongozi wakuu wa kijeshi Venezuela wanamuunga mkono Maduro, wakitangaza ahadi zao za utiifu kwenye televisheni. Waziri wa ulinzi Vladimir Padrino Lopez, mshirika mkuu wa Maduro, alipuuzilia mbali juhudi za kuwekwa serikali sambamba akisema ni sawa na mapinduzi "Nnawaonya watu wa Venezuela kuwa mapinduzi yanafanyika dhidi ya taasisi, dhidi ya demokrasia yetu, dhidi ya katiba yetu, dhidi ya Rais Nicolas Maduro, rais halali wa Jamhuri ya Venezuela" Alisema Lopez.
Kando na Marekani, sehemu kubwa ya Jamii ya Kimataifa inamuunga mkono Guaido, huku Canada na nchi nyingi za Amerika Kusini na Ulaya zikitangaza kuwa zinatambua tangazo lake la kuwa rais. Wakati huo huo, Urusi, China, Iran, Syria, Cuba na Uturuki zinaiunga mkono serikali ya Maduro.
Milio ya risasi wakati wa maandamano na uporaji imesababisha vifo vya watu 26 kati ya Jumatano na leo katika mji mkuu Caracas na kote nchini humo. Wavenezuela wengi wanasubiri Guaido ajitokeze aliko na kutoa muongozo wa hatua zinazofuata za upinzani.
Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga