MADRID: Wakimbizi waendelea kutiririka Ulaya
4 Septemba 2006Takriban wakimbizi 1,200 wamewasili Visiwa vya Kanary vya Hispania kwa njia isiyo halali katika muda wa siku mbili za nyuma.Kwa mujibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu na maafisa wa visiwa hivyo,zaidi ya wakimbizi 500 waliwasili kwa mashua za uvuvi kwenye visiwa vya Tenerife na El Hierro.Kabla ya kundi hilo,siku ya Jumamosi kiasi ya wakimbizi 674 walitokea pia nchi za Kiafrika.Visiwa vya Kanary vilivyo nje ya pwani ya Morocco na Sahara ya Magharibi,vinakabiliwa na mtiririko mkubwa wa Waafrika wanaotaka kukimbilia Ulaya.Serikali ya Hispania imeimarisha majadiliano yake na serikali za Kiafrika katika juhudi za kuzuia mmiminiko wa wakimbizi na vile vile imeziomba nchi zingine za Umoja wa Ulaya kusaidia kupiga doria baharini nje ya mipaka kwenye maji ya kitaifa.Tangu mwanzo wa mwaka huu kiasi ya Waafrika 20,000 wametua pwani za Visiwa vya Hispania.Mashirika yasio ya kiserikali yanakisia kuwa hadi watu 3,000 wamepoteza maisha yao baharini wakati wa kufanya safari hizo za hatari.