MADRID :Wahispania wafadhaishwa na hukumu zilizotolewa kwa wauaji!
1 Novemba 2007Ndugu wa watu waliouawa ama waliojeruhiwa katika mashambulio yaliyofanywa na magaidi ndani ya treni mjini Madrid wamelalamika juu ya hukumu zilizotolewa kwa magaidi waliopatikana na hatia.
Ndugu hao wamefadhaishwa baada ya mahakama kutoa adhabu ya juu kwa washtakiwa wakuu watatu tu. Watu hao , wawili wa Morocco na mmoja mhispania wamepewa adhabu ya juu ya kifungo cha maalfu ya miaka jela . Lakini chini ya sheria za Uhispania watu hao watatumikia vifungo vyao kwa muda usiozidi miaka 40.
Washtakiwa wengine 18 waliopatikana na hatia wamepewa adhabu ya vifungo visivyozidi urefu wa miaka 23.
Mshtakiwa mwengine aliedaiwa kuwa kiongozi wa magaidi alikuwa miongoni mwa watu saba walioachiwa .