MADRID: Wahamiaji wameokolewa mwambao wa Hispania
6 Oktoba 2006Kwa mujibu wa kundi la wahamiaji waliokolewa na meli ya mizigo ya Afrika ya Kusini nje ya mwambao wa Visiwa vya Kanary vya Hispania,wasafiri wenzao wapatao 20 walizama,baada ya boti waliokuwa wakisafiria kupasuka baharini.Wahamiaji walionusurika ni miongoni mwa kama Waafrika 25,000 waliofika visiwa vya Hispania katika juhudi ya kukimbia umasikini na kuingia Ulaya. Polisi wamesema,walionusurika ni watu wazima 7 na watoto 4.Kwa wakati huo huo mjini Luxembourg, mawaziri wa sheria na wa mambo ya ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya,wanajadiliana njia za kuzuia mtiririko wa wahamiaji kutoka magharibi mwa Afrika.Hispania inataka msaada zaidi wa pesa kutoka Umoja wa Ulaya kwa ajili ya walinzi wanaopiga doria katika mwambao wa nchi hiyo.Mawaziri hao wa Ulaya vile vile wanachunguza upya hatua za kuanzisha sera moja ya uhamiaji ifikapo 2010.