Madrid. Waandamanaji wailaani ETA.
14 Januari 2007Maandamano makubwa yamefanyika nchini Hispania jana Jumamosi dhidi ya kundi lenye silaha linalotaka kujitenga kwa jimbo la basque la ETA. Kiasi cha watu 175,000 waliandamana katika mitaa ya mji mkuu wa Hispania , Madrid, chini ya kauli mbiu ya amani, dhidi ya ugaidi.
Watu wengine wapatao 80,000 walijikusanya katika mji wa jimbo la Basque wa Bilbao.
Maandamano yote hayo yalikuwa kwa ajili ya kupinga shambulio la kundi la ETA katika eneo la kuegesha magari katika uwanja wa ndege wa Madrid wiki mbili zilizopita ambapo watu wawili waliuwawa.
Tangu baada ya shambulio hilo katika uwanja huo wa ndege, waziri mkuu msoshalist , Jose Luis Rodriguez Zapatero, amevunja hatua za mazungumzo ambazo zilikuwa na matumaini ya kumaliza miongo minne ya machafuko.
ETA inasisitiza kuwa shambulio hilo, ambalo imesema halikupangwa kuua mtu yeyote, halina maana ya kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano yamekwisha , lakini hoja hiyo imekataliwa na serikali.