MADRID: Raia wawili wa Ecuador waliuwawa kwenye shambulio la bomu
1 Januari 2007Matangazo
Serikali ya Ecuador imethibitisha kwamba raia wake wawili waliuwawa katika shambulio la bomu lililofanywa kwenye uwanja wa ndege wa mjini Madrid Hispania na wanamgambo wa kundi la ETA.
Hapo awali maofisa wa uokozi walihofia wanaume hao wa umri wa miaka 19 na 35, walikuwa wamefunikwa chini ya vifusi kwenye jengo la orofa la kuwekeza magari.
Watu takriban 26 walijeruhiwa katika shambulio hilo la juzi Jumamosi. Kundi la ETA la chama cha Basque limedai kuhusika na shambulio hilo.
Maelfu ya watu wamefanya maandamano mjini Madrid na miji mingine kupinga kundi hilo la ETA, wengine wakitaka serikali ya waziri mkuu Jose Luis Rodriguez Zapatero ijiuzulu.