MADRID : Kundi la ETA kuachana na suluhu
6 Juni 2007Kundi la ETA linalotaka kujitenga kwa jimbo la Basque nchini Uhispania limemaliza muda wa kusitisha mapigano wa miezi 15.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari vya Basque limeionya serikali ya Uhispania kwamba linapanga kuanzisha mashambulizi mapya katika kila pembe.Waasi hao wamesema wanaachana na makubaliano ya suluhu kutokana na kukandamizwa na serikali ya Waziri Mkuu Jose Rodrigues Zapatero.
Kundi hilo la ETA limekuwa likisisitiza kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano yalikuwa yakiendelea kutekelezwa licha ya kuuwawa kwa watu wawili katika uripuaji wa mabomu wa uwanja wa ndege wa Madrid mwezi wa Desemba mwaka jana.
Zapatero alianza kutafuta njia za kuanza mazungumzo ya amani na kundi hilo majira ya kiangazi yaliopita lakini amefuta juhudi hizo kufuatia mripuko huo.