Madrid. Hispania kurejesha wakimbizi wa maboti.
14 Septemba 2006Hispania inasema kuwa imeanza mpango wa kuyarejesha maboti ya wakimbizi nchini Senegal kutoka katika kisiwa cha Canary , licha ya upinzani kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada.
Waziri wa masuala ya jamii wa Hispania Jesus caldera hakutoa maelezo lakini gazeti la El Pais limesema wakimbizi wa kwanza 1,000 watarejeshwa kwa ndege mjini Dakar.
Waziri wa mambo ya ndani wa Senegal Ousmane Ngom amesema kuwa nchi yake katika mazungumzo na Hispania imekubali kurejeshwa kwa wakimbizi hao ambao hawana nyaraka.
Mpango wa hapo awali wa kuwarejesha wakimbizi ulisitishwa mwezi May baada ya malalamiko ya kutendewa vibaya wakimbizi hayo.
Mwaka huu wakimbizi kutoka Afrika wapatao 24,000 wamewasili katika visiwa vya Canary wakitumia maboti hafifu.
Mamia kadha wamekufa katika safari hizo zinazoambatana na hatari nyingi.
Wakati wa ulinzi wa mipaka ya umoja wa Ulaya umeanza kazi ya kulinda doria majini katika eneo la Afrika magharibi.