Wanafunzi hao - Thalib bado wanaendelea kunyanyaswa
7 Juni 2019Human Rights Watch pamoja na muungano wa mashirika ya utetezi wa haki za binadamu nchini Senegal, PPDH, wametoa ripoti hiyo ikieleza kwamba zaidi ya wanafunzi laki moja wanalazimishwa na walimu wao kwenda barabarani kuomba pesa na chakula na wamewekewa viwango vya pesa na vyakula wanavyofaa kufikisha na wasipofikisha wanadhibiwa.
Ripoti hiyo inaonyesha kwamba jumla ya wanafunzi 63 waliohojiwa miongoni mwa 88 walisema walimu wao wanawalazimisha kuomba na kwa siku wanafaa kuleta kuanzia dola senti 20 hadi dola mbili na senti ishirini. Zaidi, Mashirika hayo yaliwashuhudia baadhi ya wanafunzi walioteswa wakiwa wagonjwa, wakiwa na vidonda na makovu na hawajapokea matibabu.
Wanafunzi hao wanaofahamika kwa jina la Thalib wanaripotiwa kuendelea kunyanyaswa ambapo mwezi Februari mwaka huu mwanafunzi mmoja alikuwa anazurura usiku katika kituo cha mabasi cha Saint-Louis akihofia kurudi madrassa kwa sababu hajafikisha kiwango cha fedha alichowekewa, mwanafunzi huyo pia aliwahi kunyanyaswa kimapenzi na mwanafunzi mwenzake wa umri wa makamo. Mwezi wa nne mwalimu mmoja alikamatwa katika eneo la Mbour baada ya mwanafunzi kufariki kwa madai ya kupigwa.
Kuanzia umri wa miaka 5 wanalazimishwa kuombaomba
Thalib wa umri wa miaka 9 aliyehojiwa alisema hapendi Madrassa hizo kwa sababu wanapigwa kila wakati wasipohifadhi aya za Quran ama wasipoleta fedha, anasema wanapigwa hadi wanaona watafariki.
Human Rights Watch na PPDH walizuru mikoa minne nchini Senegal mwaka jana na mwaka huu na kuwahoji watu 150. Mahojiano yalikuwa ya ana kwa ana au kupitia simu, eslieshoji wanafunzi 88 wanaoendelea kusoma na waliomaliza pamoja na walimu, wafanyakazi na maafisa wa serikali. Wanafunzi kuanzia umri wa miaka mitano wanaombaomba katika barabara za Dakar, Saint Louis, Diourbel, Touba na Lounga.
Vile vile walizuru Madrassa 22 na vituo vya watoto 13 na kubaini wanafunzi wengi wametoroka kwa sababu ya kuteswa na kulazimishwa kuombaomba.
Mkurugenzi mshirikishi wa haki za binadamu Afrika katika shirika la Human Rights Watch, Corinne Dufka alisema maafisa wa seikali wa Senegal wanasema wamejitolea kuwalinda watoto na kusitisha kuombaomba ila unyanyasaji unaendelea na Madrassa zilizo hatari kwa wanafunzi bado zinaendelea.
Ripoti hiyo ilimtaka rais Macky Sall kuchukua hatua za kisawasawa kuwalinda maelefu ya wanafunzi katika Madrassa zinazoendeshwa bila ya muongozo.
(HRW)