Madhila yanayowapata wakimbizi wa Ogaden nchini Ethiopia.
7 Septemba 2007Macho ya Fardosa yanaonekana kama yametoka nje tangu pale alipopatwa na mkasa. Kundi la Waethiopia lilikuja nyumbani kwake mapema mwezi wa August na wanajeshi wanne walimchukua hadi chumbani kwake na kumbaka, anasema mwanamke huyo mwembamba , akimshikilia mwanae mwenye umri wa miezi tisa.
Anapanga kwenye nyumba ambamo anapaswa kulipa kiasi cha dola moja kwa siku katika eneo la Tula Absame, ambalo ni kambi ya wakimbizi iliyoko katika bandari ya Bosasso , kaskazini mwa Somalia , ambako idadi kubwa ya watu wanaokimbia hali ya machafuko katika jimbo linaloishi watu wenye asili ya Kisomali la Ogaden wanakimbilia.
Hali mbaya ya maisha katika kambi ya Tula Absame pamoja na hali ya joto kali si kikwazo kwa mamia ya wakimbizi wa Ogaden wanaojitayarisha kwa ajili ya safari ya baharini yenye mashaka, katika ghuba ya Aden kutafuta maisha mapya na bora nchini Yemen na kwingineko.
Majeshi ya Ethiopia yameanzisha msako mkubwa katika jimbo hilo la Ogaden. Lengo lao kuu ni kundi la waasi wa Ogaden National Liberation Front ONLF, kundi lililoundwa miongo miwili iliyopita wakitaka uhuru wa jimbo lao kutokana na kile wanachosema ni kutengwa na utawala wa mjini Addis Ababa.
Lakini madai ya ONLF na ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu zimeonyesha hali ya wasi wasi kuwa adhabu za jumla zimesambaa na malipizo ya kisasi dhidi ya raia yanafanyika katika jimbo la Ogaden, jimbo ambalo liko chini ya udhibiti mkubwa wa jeshi la Ethiopia.
Fardosa anasema kuwa kaka zake wawili ambao walikuwa wanachama wa kundi la waasi wa ONLF walinyongwa katika mit. Anaongeza kuwa hii ni hali mbaya kabisa inayotokea nchini Ethiopia.
Osman Hassan Ahmed , mwenye umri wa miaka 27 kutoka mji wa Werder ulioko mashariki mwa jimbo la Ogaden aliwasili Bosasso mnamo Septemba mosi. Anasema kuwa mgahawa wake aliokuwa akiuza chai ulifungwa na wanajeshi mwezi wa Februari na alikuwa akishutumiwa kuwafadhili waasi wa ONLF. Mapema mwezi Julai alikamatwa pamoja na marafiki zake wawili na alifanikiwa kutoroka kutokana na usaidizi wa ndugu zake walioko jeshini.
Wakimbizi wa kutoka Ogaden wanashanga kuhusu ukimya ulioko katika jamii ya kimataifa kuhusu madhila yao katika jimbo lao.