Maoni:Kadhia ya mauaji ya walemavu wa ngozi Tanzania
6 Machi 2015Watoto wawili wenye ulemavu wa ngozi wametoweka katika miezi miwili iliyopita licha ya serikali kuwapiga marufuku wapiga ramli wanaoshutumiwa kwa kuchochea mashambilizi ya walemavu wa ngozi kupata sehemu za miili yao zinazotumiwa kutengeneza hirizi na dawa zinazoaminiwa kuwa na nguvu za kuleta bahati nzuri na utajiri.
Februari mwaka huu polisi walipata maiti ya kijana Yohana Bahati aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja, siku chache baada ya genge lililokuwa limejihami na silaha kumteka nyara kutoka nyumbani kwao katika eneo la Geita, kaskazini magharibi ya Tanzania. Mikono yake na miguu yake ilikuwa imenyofolewa.
Yohana Bahati alikuwa mtoto wa pili kutekwa katika kipindi cha miezi miwili katika kanda ya ziwa nchini Tanzania, ambako inakadiriwa watu 75 wenye ulemavu wa ngozi wameuwawa tangu mwaka 2000, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. Msichana wa umri wa miaka minne alitekwa nyara mwezi Desemba mwaka uliopita na mpaka sasa hajulikani aliko.
Katika kipindi chetu cha Maoni mbele ya meza ya duara kinachoongozwa na mwenyekiti Josephat Charo, tunazungumzia kadhia ya mauaji ya walemavu wa ngozi nchini Tanzania, changamoto na mashaka yanayowakabili watu hawa hata katika nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Kusikiliza maoni bonyeza alama ya spika za masikioni hapo chini.