Hata safari za abiria zitaathirika
4 Mei 2015"Mzozo wa shirika la safari za reli la Ujerumani Deutsche Bahn watu wanashindwa kuuelewa" amesema waziri wa uchumi,Sigmar Gabriel wa kutoka chama cha Social Democratic SPD ,akisikitika kwamba mgomo huu wa wiki nzima unaoanza hii leo unawaathiri vibaya sana abiria,shirika lenyewe la Deutsche Bahn na shughuli jumla za kiuchumi nchini Ujerumani.
Waziri wa usafiri wa serikali kuu Norbert Barthle wa kutoka chama cha kihafidhina cha Christian Democratic-CDU amekosoa kile alichokiita "hali isiyovumilika".
Mzizi wa fitina ni suala la wakala na masaa ya kazi
Shirika linalopigania haki za madereva wa treni GDL linazozana tangu mwaka mmoja uliopita pamoja na uongozi wa shirika hili la Deutsche Bahn linalomilikiwa na serikali.Mzizi wa fitina unahusu masuala ya nani aliwakilishe shirika hilo katika majadiliano kuhusu nyongeza za mishahara na masaa ya kazi.Madai hayo yanapingwa na shirika la Deutsche Bahn.
Shirika la madereva wa treni GDL na kiongozi wake mkakamavu Claus Weselsky wameshaitisha migomo mara saba tangu mwezi wa julai mwaka jana.Wa nane ni huu ulioanza saa tisa za mchana hii leo kwa kusitishwa shughuli za kusafirisha mizigo na ambao Claus Weselsky anasema utakuwa mgomo wa muda mrefu zaidi kuwahi kushuhudiwa katia historia ya shirika la safari za reli la Ujerumani Deutsche Bahn.
Mgomo wa safari za treni za abiria unaanza usiku wa manane wa leo kuamkia kesho.Mgomo huo utaendelea hadi saa moja asubuhi jumapili ijayo.
Shirika la safari za reli la Ujerumani linasafirisha abiria milioni tano na laki tano pamoja na tani 607.000 za bidhaa kwa siku pekee nchini Ujerumani bila ya kuzitaja safari kuelekea maeneo yote muhimu barani Ulaya kuanzia kaskazini hadi kusini na mashariki hadi magharibi.
Kansela Merkel asihi mzozo umalizike haraka
Wanaviwanda wanapiga makelele,wanasema mgomo huu wa wiki nzima utailisha hasara ya mamilioni ya Euro sekta ya kiuchumi nchini Ujerumani.
Migomo iliyotangulia imeshaligharimu shirika hilo dala milioni 200.
Deutsche Bahn litatangaza ratiba mpya na kuahidi thuluthi moja ya safari za masafa marefu za treni na kati ya asili mia 15 hadi 60 ya safari za kimkoa zitaendelea kama kawaida.
Kansela Angela Merkel amezungumzia mzigo kwa wasafiri na wanaviwanda na kuwaasihi madereva wa treni na shirika la Deutsche Bahn wamalize haraka mzozo wao.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel