Madereva wa treni Ujerumani waanza mgomo mrefu kabisa
24 Januari 2024Mgomo huo ulioanza usiku wa kuamkia Jumatano (Januari 24) na kuendelea hadi Jumatatu ijayo ni wa duru ya nne katika mvutano baina ya Shirika la Reli la Ujerumani (DB) na Chama cha Madereva wa Treni (GDL).
Mgomo huo unatarajiwa kusababisha usumbufu kwa wasafiri na hadi sasa hakuna ishara thabiti za kuonesha iwapo pande mbili hizo zitarejea kwenye mazungumzo.
Soma zaidi: Mgomo wa treni Ujerumani huenda ukagharimu euro bilioni 1
Kiongozi wa GDL, Claus Weselsky, alisema wao wapo tayari kufikia mwafaka juu ya mishahara na masaa ya kazi.
"Shirika la Reli lazima litoe mapendekezo ya kuongeza mishahara. Sisi tuko tayari kufikia muafaka. Na ikiwa watazingatia hilo la kuongeza mishahara, basi na sisi tunaweza kurudi kwenye meza ya mazungumzo. Lakini ikiwa hakuna chochote kitakachotokea kufikia siku ya Ijumaa, hatutasita kwenda katika hatua inayofuata ya mapambano yetu." Alisema mkuu huyo wa madereva wa treni.
Soma zaidi: Deutsche Bahn yapendekeza mpango mpya wa mishahara
Msemaji wa Shirika la Reli ameeleza kuwa mgomo huo ni hatua nyingine ya usumbufu mkubwa nchini Ujerumani kote na amewataka wajumbe wa GDL warejee kwenye meza ya mazungumzo.