1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watalii 29 Wajerumani wafariki katika ajali Madeira

18 Aprili 2019

Kisiwa cha Ureno cha Madeira kimeanza siku tatu za maombolezo baada ya watalii 29 raia wa Ujerumani kufa katika ajali ya basi. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametuma risala zake za rambirambi kwa familia za wahanga.

https://p.dw.com/p/3H1Dd
Portugal Busunglück auf Madeira
Picha: Getty Images/AFP/R. Silva

Basi walimokuwa wakisafiria watalii hao liliacha barabara na kubingiria kwenye mteremko na hatimaye kuigonga nyumba moja karibu na mji wa Canico kisiwani Madeira. Picha zilizochukuliwa na kifaa cha kupigia picha aina ya "drone" zilionyesha basi hilo lililoharibiwa vibaya likiwa limeliegemea jengo la nyumba hiyo kwenye kilima, upande wake wa juu ukiwa umeharibiwa na kioo cha mbele kikiwa kimevunjika.

Wafanyakazi wa timu ya uokozi waliwahudumia abiria waliojeruhiwa katika eneo ambapo basi lilisimama, baadhi yao wakiwa na bendeji zilizojaa damu kichwani na nguo zilizolowa damu, huku wengine wakionekana kuwa na majeraha mabaya sana. Ilse Berardo, mchungaji wa kanisa la kiinjili la Ujerumani kisiwani Madeira amekiambia kituo cha televisheni cha Ujerumani, RTL, kwamba waliojeruhiwa wanakabiliwa na mshtuko, wakikumbuka waliyoyashuhudia wakati wa ajali. Mwanamke mmoja alisema amempoteza mpenzi wake katika ajali hiyo.

Maafisa wamesema wengi wa waliokufa wana umri kati ya miaka 40 na 50. Wanaume 11 na wanawake 18 ni miongoni mwa wahanga na wote ni Wajerumani. Walikuwa miongoni mwa watalii zaidi ya milioni moja wanaovitembelea visiwa vilivyoko katika bahari ya Atlantiki nje ya pwani ya Morocco kila mwaka, wakivutiwa na hali yake ya hewa ya kitropiki na muonekano wa mandhari yake.

Portugal Busunglück auf Madeira
Basi lililopata ajali Funchal, MadeiraPicha: Imago Images/GlobalImagens/R. Silva

Merkel atuma risala za rambirambi

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, alituma risala zake za rambirambi kwa familia za wahanga wa ajali hiyo. Merkel ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter, "Ni kwa huzuni na masikitiko makubwa kwamba ninawafikiria wenzetu na watu wengine watano walioathiriwa na ajali ya basi huko Madeira." Aliwashukuru maafisa wa uokoaji na madaktari wa Madeira kwa juhudi zao na kusema afisi ya wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani na wafanyakazi wake nchini Ureno wanashirikiana na maafisa wa Madeira kuwasaidia walioathiriwa na ajali hiyo.

Rais wa Ureno, Marcelo Rebelo de Sousa, aliimabia televisheni ya taifa anatoa pole na kuonyesha mshikamo wa watu wa Ureno katika kipindi hiki kigumu cha huzuni, hususan kwa familia za wahanga ambao alifahamishwa ni Wajerumani. Naye waziri Mkuu wa Ureno, Antonio Costa, aliandika katika twitter kwamba amewasiliana kansela Merkel kutuma risala zake za rambirambi.

Chumba cha muda cha kuhifadia maiti kiliwekwa katika uwanja wa ndege swa Funchal. Timu za madaktari watasafirishwa kwa njia ya ndege hadi kisiwani humo kutoka mjini Lisbon kufanya uchunguzi wa maiti.

afpe, dpa, reuters