Madaktari: Afya ya Biden ni njema
17 Februari 2023Majibu ya vipimo vya kitabibu alivyofanyiwa rais wa Marekani Joe Biden yameonyesha kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 80 ni buheri wa afya na anaweza kuyatekeleza vyema majukumu yake. Majibu hayo ya baada ya uchunguzi wa masaa matatu yalisubiriwa kwa shauku kwa kuzingatia azma ya rais huyo kugombea muhula wa pili katika uchaguzi wa mwakani. Biden alichukuliwa vipimo katika hospitali ya kijeshi ya Walter Reed iliyoko Bethesda, Maryland ambapo matatizo madogo madogo yamegunduliwa lakini hakukutwa na madhara ya muda mrefu yatokanayo na maambukizi ya UVIKO ambayo yalimsibu mara mbili. Katika barua iliyochapishwa katika tovuti ya Ikulu ya Marekani, The White House, Daktari wa Rais Biden, Kevin O'Connor amesema rais huyo ana afya njema na nguvu za kutosha kuendesha majukumu yake kama kiongozi wa serikali na amiri mkuu wa jeshi.