1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mada za kila aina katika hotuba ya rais Obama

13 Februari 2013

Rais Obama ajitokeza mkakamavu katika hotuba yake kwa taifa iliyoyataja matatizo ya kila aina yanayoikabili nchi hiyo,bila ya kutoa mapendekezo ya vipi marekebisho yatapatikana -wanasema wahariri

https://p.dw.com/p/17dJ5
Ripota wa DW katika mji mkuu wa Marekani,Washington:Christina BergmannPicha: DW

Bora asingesema mengi! Badala ya kuzungumzia zaidi kuhusu baadhi ya masuala, rais Barack Omaba ameorodhesha katika hotuba yake takriban mada zote za siasa ya ndani ambazo ama zinahitaji kurekebishwa au kufanyiwa mageuzi. Na mada hizo ni nyingi kweli kweli - na ni ushahidi kwamba hali ya taifa hainawiri hivyo - kama alivyotamka mwanzoni mwa hotuba yake.

Matumizi ya serikali yanabidi yapunguzwe - tiba, bima ya afya kwa wazee - inaabidi ifanyiwe marekebisho na nakisi katika kodi za mapato ipunguzwe. Hiyo ndio orodha ya mambo yanayostahiki kutekelezwa, anasema rais Obama. Nafasi za kazi zinahitajika na hasa viwandani, mafunzo ya kazi yaimarishwe na mabadiliko ya tabia nchi yaepukwe. Miundo mbinu iliyochakaa ifanyiwe marekebisho, sawa na sera zinazowahusu wahamiaji na kurahisisha utaratibu wa kupiga kura. Na sheria ya kumiliki silaha izidishwe makali.

Upinzani wategemewa kutoka baraza la Congress

Yote haya mtu anaweza kusema watu wameshawahi kuyasikia. Rais hakutoa mapendekezo halisi kwa mfano vipi kiwango cha chini cha mshahara kitaongezwa na kufikia dala tisa. Na amesema yuko tayari kupitisha kanuni pindi baraza la Congress kwa mfano likishindwa kufikia makubaliano ya jinsi ya kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Na hapo hasa ndipo tatizo lenyewe hasa linapokutikana. Baraza la wawakilishi linadhibitiwa kama zamani na wanachama wa Republican na, tukitenga suala la mageuzi ya sheria za uhamiaji, hawaonyeshi dalili ya kutaka kufikia maridhiano.

Siasa ya nje haikupewa umuhimu mkubwa

Na siasa ya nje je? Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2009, amezungumzia kwa ufupi tu. Wanajeshi wa Marekani wataendelea kuihama Afghanistan katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, wanajeshi 34 elfu watakuwa wamesharejea nyumbani. Mwisho mwa mwaka 2014 zoezi la kuwarejesha nyumbani wanajeshi wa Marekani litakamilika. Rais Obama amesema wazi kabisa kwamba siku za mbele kupelekwa wanajeshi wa Marekani katika maeneo ya mizozo itakuwa njia ya mwisho kabisa -hata katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la al Qaida.

Obama ambaye mwezi ujao ataitembelea Israel, amesisitiza anaunga mkono kudhaminiwa usalama wa nchi hiyo, lakini kauli hiyo imegeuka kuwa ya lazima kutolewa na rais wa Marekani kwa sababu hataki kuzongwa na lawama. Onyo limetolewa na Barack Obama kwa Korea ya kaskazini pale Obama alipolitaja jaribio la silaha za kinyuklia na pia Iran. Obama hakusahau kugusia kwamba mradi wake wa kutuma madege yasiyokuwa na rubani unaambatana na sheria na kwamba  nchi yake na Urusi zimedhamiria kupunguza silaha za kinyuklia katika nchi zao.

Katika hotuba yake rais ameonekana, mkakamavu na amepania zaidi kuliko alivyokuwa miaka ya nyuma. Lakini si ajabu kwa sababu anajua huu ni mhula wake wa mwisho na hawezi kuchaguliwa tena.

Mwandishi: Bergmann Christina/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Josephat Charo