Macron, Scholz watoa wito wa kurekebisha uhusiano na China
13 Aprili 2024Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz wametoa wito wa kurekebisha uhusiano wa kibiashara kati ya Ulaya na China. Wito huo umetolewa kabla ya Kansela Scholz kufanya ziara mjini Beijing mwishoni mwa juma hili.
Viongozi hao wawili, pia walijadili athari za vita vya Ukraine kwa usalama wa Ulaya, katika mazungumzo kwa njia ya video siku ya Ijumaa.
Kansela Scholz anaelekea China kwa ziara ya siku tatu wakati ambapo nchi za Magharibi zikizidi kuelezea wasiwasi juu ya mienendo ya China katika biashara na ukaribu wake na Moscow.
Umoja wa Ulaya unaishutumu China, kuiingiza Ulaya bidhaa za ruzuku zinazouzwa kwa bei ya chini. Kulingana na ofisi ya Macron, viongozi hao wamesisitiza uungaji mkono usioyumba kwa Ukraine na kuendelea kuisaidia kijeshi.