Macron atambua dhima ya Ufaransa katika mauaji ya Rwanda
27 Mei 2021Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron siku ya Alhamis ametambua dhima ya nchi yake katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, kuanzia kuunga mkono utawala, hadi kupuuza maonyo juu ya mauaji yaliokuwa yanakaribia. Macron amesema Ufaransa ilikuwa na jukumu la kukiri mateso iliyoyasababisha kwa watu wa rwanda.
Katika ziara yake Rais Macron amesema kuwa Ufaransa haikuhusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, lakini akiongeza kuwa kwa muda mrefu Ufaransa imekuwa ikithmini sana ukimya kuliko ukweli. Macron amesema anatambua mapungufu ya Ufaransa katika mauaji hayo yaliyowalenga hasa watu wa jamii ya Wahutu
Ziara hiyo ya Macron imekuja kufuatia kuchapishwa mwezi Marchi ripoti ya jopo la uchunguzi la Rwanda iliyosema kwamba tabia za kikoloni zimewafumba macho maafisa wa Ufaransa na serikali ya nchi hiyo inabeba dhamana kubwa kwa kutotambua mapema mauaji yaliyotokea.
Hata hivyo ripoti hiyo iliiepusha kuihusisha moja kwa moja Ufaransa katika mauaji ya zaidi ya watu 800,000 wa jamii ya kabila la Watusti na wahutu waliokuwa na msimamo wa wastani.Nchini Rwanda,rais huyo wa Ufaransa amesema nchi yake haikuhusika lakini pia haikuwasikiliza wale waliotahadharisha kuhusu hali ya Rwanda.
Ziara ya kwanza tangu 2010
Macron ndiye kiongozi wa kwanza wa Ufaransa tangu 2010 kuitembelea Rwanda ambayo kwa muda mrefu imeituhumu Ufaransa kwa kutochukua hatua wakati wa mauaji ya kimbari ya Watutsi. Miaka kadhaa ya kunyosheana vidole, hatimaye ilifikia kikomo mnamo mwezi Machi pale tume iliyoteuliwa na Rais Macron ilipoituhumu Ufaransa kwa jukumu lake katika umwagikaji huo wa damu.
Tume hiyo iliyokuwa inaongozwa na wanahistoria, katika matokeo yake ilisema Ufaransa ambayo ilikuwa na mahusiano ya karibu na Wahutu waliokuwa madarakani wakati huo na waliohusika na mauaji hayo, kuwa ilifumbia macho maandalizi ya mauaji hayo ya halaiki. Tume hiyo lakini haikupata ushahidi wa Ufaransa kuhusika katika mauaji hayo. Ufaransa imekiri yote yaliyotajwa na tume hiyo.
Kwa Rais Paul Kagame ambaye aliongoza upinzani wa Watutsi dhidi ya mauaji hayo jambo lililopelekea kusitishwa kwa mauaji hayo na pia kama mtu ambaye amekuwa akiituhumu Ufaransa tangu awali, ripoti hiyo ilikuwa kama mwanzo mpya. Katika ziara yake ya Ufaransa, Kagame ambaye wakati mmoja alikata kabisa mahusiano ya Rwanda na Ufaransa, alisema ripoti hiyo ilitoa nafasi ya Ufaransa na Rwanda kuwa na mahusiano mazuri.
Maafisa wa Ufaransa wanasema Macron anaweza kutumia ziara hii kumtaja balozi wa Ufaransa nchini Rwanda na kujaza pengo lililoachwa wazi tangu mwaka 2015. Lakini wengine Rwanda wanaitaka Ufaransa ikiri na kuomba radhi rasmi kwa kushindwa kuzuia mauaji ya Wanyarwanda 800, 000 kati ya Aprili na Julai 1994. Watakuwa wanasikiliza kwa makini rais huyo wa Ufaransa atakapokuwa akitoa hotuba yake baadaye leo katika Makumbusho ya mauaji hayo ya halaiki.
Kiongozi wa mwisho
Rais wa mwisho wa Ufaransa kuizuru Rwanda alikuwa Nikolas Sakorzy ambaye alijaribu kuuanzisha mjadala huo kuhusiana na mauaji hayo kwa kukiri kwamba Ufaransa ilifanya makosa makubwa na kujitia upofu katika suala hilo. Hilo halikuwaridhisha Wanyarwanda na mahusiano kati ya nchi hizo mbili yakaendelea kuzorota.
Sasa Macron amejiwasilisha kama rais wa kizazi kipya kilichokuja baada ya enzi za ukoloni na kwamba haogopi kukiri kuhusiana na makosa yaliyofanyika zamani. Alipokuwa akifanya kampeni za urais, Macron mwenye miaka 43 alisema ukoloni wa Ufaransa kwa Algeria lilikuwa ni "kosa la jinai" jambo lililowaghadhabisha mno Wafaransa Wahafidhina ambao kwa muda mrefu walikuwa wanachukulia ukoloni kama kitu kizuri kuwahi kufanyika.
Kuhusiana na suala la uporwaji wa kazi za sanaa za Waafrika katika kipindi cha ukoloni, Macron ameonekana kuwa tofauti kidogo na watangulizi wake kwa kukubali maovu yaliyotendwa na Ufaransa kwa nchi za Afrika. Ameahidi kurudisha kazi za sanaa zilizoporwa Benin na Senegal.
Wachambuzi wanasema jambo hili analofanya Macron linalenga kujikosha tu mbele ya kizazi kipya cha Waafrika.
Ili kujaribu kuyazima madai ya ukoloni mambo leo dhidi ya Ufaransa kwa nchi zinazozungumza lugha hiyo, Macron amejaribu kuanza kuanzisha mahusiano na nchi zinazozungumza Kiingereza ambazo kitamaduni haziko kwenye eneo la mamlaka ya Ufaransa.
Baada ya kutoka Rwanda, rais huyo ataelekea Afrika Kusini ambako atafanya mazungumzo na Rais Cyril Ramaphosa kuhusiana na mapambano dhidi ya Covid-19 na athari zake kwa uchumi wa dunia.