Macron asema China ina 'jukumu kubwa' mzozo wa Ukraine
6 Aprili 2023Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema China ina jukumu kubwa la kurejesha amani nchini Ukraine. Macron ameyasema hayo kwenye mazungumzo mjini Beijing na Rais wa China Xi Jinping ambapo wanatarajia kuangazia vita vya Urusi nchini Ukraine.
Kwa upande wake, Rais Xi aliyasifia mahusiano baina ya nchi zao mbili kwamba yanapitia kipindi chenye mabadiliko makubwa ya kihistoria.
Viongozi hao wawili wanatarajiwa kuzungumza na Xi kuhusu masuala ya biashara, mabadiliko ya tabianchi na bioanuai pamoja na usalama wa chakula. Kiongozi huyo wa China alimpokea Macron kwa heshima za kijeshi.
Macron ameelezea pia kuhusu mkutano wa kilele juu ya mkataba mpya wa kifedha utakaofanyika mjini Paris mwezi Juni, ambapo China itakuwa na jukumu muhimu. Lengo kuu likiwa ni kufadhili mapambano dhidi ya umaskini na kuandaa mpito wa kiekolojia.