1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron alaani mauaji ya waandamanaji wa Algeria mwaka 1961

17 Oktoba 2021

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameyalaani mauaji yaliyofanywa na polisi wa Ufaransa dhidi ya waandamanaji wa Algeria kuwa “uhalifu”. Hata hivyo hakuomba radhi rasmi.

https://p.dw.com/p/41mPE
Frankreich Paris | Emmanuel Macron bei den Gedenkfeierlichkeiten in Colombes
Picha: Rafael Yaghobzadeh/AP Photo/picture alliance

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron siku ya Jumamosi alishutumu vikali mauaji yaliyofanywa na polisi mjini Paris dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakitaka uhuru wa Algeria, ambao wakati huo ilikuwa koloni la Ufaransa.   

Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Macron, muda mfupi baada ya kuhudhuria kumbukumbu ya miaka 60 tangu mauaji hayo yalipofanyika ilisema Macron "alitambua: kwamba uhalifu uliofanyika usiku huo chini ya aliyekuwa mkuu wa polisi wakati huo Maurice Papon hayawezi kukubalika katika jamhuri.” Macron alihudhuria maadhimisho hayo lakini hakutoa hotuba kwenye hafla hiyo.

Soma pia: Algeria yamrudisha nyumbani balozi wake kutoka Ufaransa

Maandamano hayo ya Oktoba 17, 1961, yalifanyika katika mwaka wa mwisho wa machafuko ya juhudi za Ufaransa kujaribu kuchukua tena udhibiti wa koloni lake Algeria.

Macron akosa kuomba radhi rasmi

Japo hakuomba radhi rasmi, maneno ya Macron yameenda zaidi ya yaliyotolewa na mtanguizi wake Francois Hollande ambaye mnamo mwaka 2012 alitambua tu kwamba "waandamanaji wa Algeria waliuawa wakati ukandamizaji na umwagikaji damu ulitokea maandamano yalipokuwa yakizimwa.” Waandamanaji kadhaa pia walitiwa nguvuni katika- maandamano hayo ya amani.

Rais Emmanuel Macron ndiye rais wa kwanza wa Ufaransa kuhudhuria kumbukumbu za mauaji hayo ya Waandamanaji wa Algeria mjini Paris tangu yalipofanyika 1961.
Rais Emmanuel Macron ndiye rais wa kwanza wa Ufaransa kuhudhuria kumbukumbu za mauaji hayo ya Waandamanaji wa Algeria mjini Paris tangu yalipofanyika 1961.Picha: Rafael Yaghobzadeh/AP Photo/picture alliance

Macron ndiye rais wa kwanza wa Ufaransa kuhudhuria kumbukumbu hizo zilizohudhuriwa pia na wahanga, wanaharakati na mashujaa wa Algeria waliopigania uhuru.

Soma pia:Algeria: Miaka 60 tangu majaribio ya nyuklia ya Ufaransa

Baada ya kushuhudia shada ya maua ikiwekwa, Macron alizungumza na baadhi ya Waalgeria waliohudhuria.

Waalgeria waliandamana kupinga marufuku waliyowekewa ya kutembea nje ili kulizuia vuguvugu la FLN kutochanga fedha baada ya kufanya misururu ya mashambulizi dhidi ya maafisa wa polisi wa Ufaransa.

Licha ya marufuku hiyo, zaidi ya waandamanaji 25,000 waliandamana kupinga hatua hizoza Ufaransa nchini Algeria. Takriban raia 12, 000 wa Algeria walikamatwa wakati wa maandamano hayo.

Ukandamizaji wa polisi

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 200 waliuawa wakati polisi walipovunja maandamano hayo ya Oktoba 17, 1961.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 200 waliuawa wakati polisi walipovunja maandamano hayo ya Oktoba 17, 1961.Picha: AFP

Haijulikani wazi idadi kamili ya watu waliouawa wakati wa maandamano usiku huo, lakini baadhi ya wanahistoria wamesema makumi kwa makumi ya watu waliuawa. Hii ni licha ya takwimu rasmi ya awali iliyodai kuwa ni watu watatu pekee ndio waliuawa.

Baadhi ya wanaharakati wanahofia mamia ya watu waliuawa, wakiwemo waandamanaji ambao maafisa wa polisi waliwatupa katika mto Seine na kufa maji. Wengine walipigwa hadi kufa au waliuawa kwa kupigwa risasi.

Matukio ya Oktoba 17 yalisababisha vurugu za wiki kadhaa. Kwa miongo mingi, maovu hayo yamekuwa yakifichwa. Miili ya waathiriwa wengi haijapatikana hadi leo.

Baadaye, iligunduliwa kwamba Papon ambaye alikuwa mkuu wa polisi wakati huo, alikuwa mshirika wa utawala wa kinazi wakati wa Vita Vikuu Vya Pili ulimwenguni, jambo lililoongeza aibu zaidi kwenye matukio ya siku hiyo.