1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macky Sall kuanza mazungumzo kumaliza mkwamo wa kisiasa

26 Februari 2024

Rais Macky Sall wa Senegal anatarajiwa kuanza mazungumzo ya kumaliza wiki kadhaa za machafuko ya kisiasa na pia kuamua tarehe mpya ya uchaguzi wa urais uliocheleweshwa.

https://p.dw.com/p/4cuCO
Rais Macky Sall wa Senegal.
Rais Macky Sall wa Senegal.Picha: DW/AFP

Sall alipendekeza kuwa wagombea wote wa awali katika kinyang'anyiro cha urais wajumuishwe kwenye mazungumzo hayo, pamoja na wale ambao walikuwa wameondolewa kwenye orodha ya kugombea.

Pia aliwaalika viongozi wa asasi za kiraia, dini na kijamii katika mkutano huo uliopangiwa kufanyika siku ya Jumatatu (Februari 26).

Lakini wagombea 16 kati ya 19 walioidhinishwa na Baraza la Katiba walisema wasingehudhuria mkutano huo.

Muungano wa zaidi ya mashirika 100 ya kiraia unaojulikana kama The Aar Sunu Election pamoja na watu binafsi wanaopinga kucheleweshwa kwa uchaguzi, pia walitangaza kususia mazungumzo hayo.

Pande zote zinajumuisha sehemu ya vuguvugu linalotaka kufanyika kwa uchaguzi kabla ya Aprili 2, wakati muda wa Sall madarakani utakapomalizika.

Baadhi ya watu wanahofia uwezekano wa ombwe la uongozi iwapo Sall ataachia madaraka kabla ya kupatikana kwa mrithi wake.