1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mackenzie akataa kufika mahakamani Mombasa

14 Machi 2024

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya Shakahola, Paul Mackenzie, amekataa kuhudhuria kusikilizwa kwa kesi ya ugaidi inayomkabili yeye na wengine 94. Mwanasheria wake alijaribu kumshawishi akaonekane mahakamani bila mafanikio.

https://p.dw.com/p/4dWK8
Afrika Mombasa/ Paul Mackenzie
Mshukiwa mkuu wa mauaji ya Shakahola, Paul MackenziePicha: Halima Gongo/DW

Kusikilizwa kwa Kesi yake kulikuwa ni kwa ajili ya maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka kupinga kuachiliwa huru kwa washukiwa hao 95 wa mauaji ya halaiki katika msitu wa Shakahola huko Pwani ya Kenya. 

Wakili wa Mackenzie Wycliffe Makasembo, alimwambia Hakimu Mkuu wa mahakama ya Mombasa Leah Juma kwamba mteja wake Mackenzie alikuwa anafungiwa peke yake na washukiwa wengine na kusema kuwa uongozi wa gereza unawabagua.

Kenya kuugeuza msitu wa Shakahola kuwa kituo cha kumbukumbu

Makasembo pia aliiambia mahakama kwamba mteja wake Mackenzie alieleza kuwa na hofu ya kutekwa nyara. Hata hivyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Peter Kiprop, Mshauri Mkuu wa Mashtaka Anthony Musyoka na Mshauri Mkuu wa Mashtaka Peris Ongega walipinga ombi la kuahirisha kesi wakitaja madai ya Mackenzie kama njama za kuchelewesha kesi.

Hakimu Mkuu Leah Juma pia aliagiza Kituo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Ugaidi (NCTC) kuandaa ripoti za kisaikolojia kuhusu kila mmoja wa washitakiwa wa Shakahola. Mahakama itatoa maelekezo zaidi ya Kesi hii tarehe 27 Machi mwaka huu wa 2024.
 huko Pwani ya Kenya